SERIKALI YAZINDUA MWONGOZO WA MAFUNZO YA UJUZI KAZINI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, January 24, 2026

SERIKALI YAZINDUA MWONGOZO WA MAFUNZO YA UJUZI KAZINI

Na Godwin Myovela, Iringa

Mkoa wa Iringa jana umeshuhudia kufungwa kwa mafunzo ya wakulima na wasindikaji wadogo na uzinduzi wa Mwongozo wa Uratibu wa Mafunzo ya Kuongeza Ujuzi kwa Wafanyakazi nchini, hatua inayolenga kuongeza tija, ajira na thamani ya mazao ya kilimo.

Akifunga mafunzo hayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Riyadh Kisuo, aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao, akisisitiza matumizi ya ujuzi walioupata ili kuboresha uzalishaji na kipato.

Jumla ya wahitimu 1,062 kutoka mikoa ya Iringa, Singida, Dodoma na Mbeya wamepatiwa mafunzo ya usindikaji na kuongeza thamani ya mazao mbalimbali yakiwemo nyanya, mchicha, alizeti, zabibu na parachichi.

Katika hafla hiyo, Kisuo pia alizindua Mwongozo wa Uratibu wa Mafunzo ya Kuongeza Ujuzi kwa Wafanyakazi nchi nzima, unaolenga kuhakikisha mafunzo yanazingatia mahitaji halisi ya soko la ajira na uzalishaji.

Awali, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Godwin Mpelumbe, alisema hadi sasa watanzania 157,847 wamenufaika na mafunzo hayo huku wahitimu 250 wakitoka mkoa wa Iringa.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini TARI, Dk. Thomas Bwana, ambao wamepewa dhamana ya kuendesha mafunzo hayo, alisema taasisi hiyo inaendelea kusambaza teknolojia bunifu na tafiti za kilimo ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa uzalishaji wa kilimo nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi wa TPSF, Gasper Mdee, alisema changamoto ya kuongeza thamani bado ni kubwa kutokana na wengi kujikita kwenye mazao ghafi, akisisitiza umuhimu wa usahihi katika uchakataji, ufungashaji, uundaji wa chapa na usafirishaji.

Akizungumzia mwongozo huo, Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Rehema Ludanga, alisema utasaidia kuweka mifumo iliyo wazi na kuoanisha mahitaji ya soko la ajira na uzalishaji sambamba na uwajibikaji wa mfanyakazi.

Naye Mwakilishi wa ATE, Selestine Leonard, aliwataka waajiri kuzingatia vimo vya chini vya mishahara ambavyo utekelezaji wake umeanza mwezi huu.

Kwa niaba ya wananchi wa kata za Ikokoto, Itunda, Mazombe na Mbigiri, Meneja wa IFCU Iringa, Tumaini Lupola, aliishukuru Serikali kwa kuendesha mafunzo hayo, akisema yamerahisisha upatikanaji wa tija na kuongeza kipato cha wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad