Mkurugenzi wa Usambazaji Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (UWASA), Mhandisi Salum Ngumbi akizungumza na wanahabari wa mkoa wa Tanga hawapo pichani.
............................................
Na Mashaka Kibaya,Tanga
KATIKA kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa Wateja wake, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) inatekeleza mradi mkubwa wa kuboresha hali ya upatikanaji huduma ya maji Tanga awamu ya tatu kupitia ufadhili wa Hatifungani ya Kijani maarufu kama ''Tanga Water Green Bond'' unaotarajiwa kukamilika mwezi Machi 2026.
Imeelezwa kuwa pindi mradi huo utakapokamilika utatoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Jiji la Tanga pamoja na Miji ya Muheza, Pangani na Mkinga.
Hivi karibuni (Disemba 23,2025) Waandishi wa habari wa Mkoa wa Tanga wakiwa sehemu ya Wadau, walipata fursa ya kutembelea mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Tanga (Tanga UWASA).
Mhandisi Salum Ngumbi, ni Mkurugenzi wa usambazaji maji na Usafi wa mazingira, amesema kuwa mradi wa Hatifungani ya kijani unagharimu Shilingi Bilioni 53.12 na ukikamilika utaongeza kiwango cha uzalishaji na usambazaji maji kutoka mita za ujazo 45,000 hadi kufikia mita za ujazo 60,000 kwa siku.
Alieleza kuwa kupitia utekelezaji wa mradi huo miundombinu ya usambazaji maji itaboreshwa ambapo mabomba makubwa yenye kipenyo cha mm 600 kwa urefu wa kilomita 6.4 yatalazwa kutoka kituo cha kusukuma maji Mabayani hadi Mowe mahali ulipo mtambo unaotumika kuzalisha maji kwa lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji na usambazaji maji.
Aidha kunafanyika upanuzi wa kituo cha kusafisha na kutibu maji cha Mowe, ujenzi wa tangi la kuhifadhia maji lenye ukubwa wa mita za ujazo 35,000 pamoja na kuongezwa mtandao wa usambazaji maji maeneo ya pembezoni na maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma.
Vilevile kutafanyika ukarabati wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka, kufungwa dira 10,000 za malipo kabla ikiwa ni pamoja na kuimarisha shughuli za utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Katika ziara hiyo ya wanahabari alikuwepo Mashaka Mhando, Mwandishi wa Gazeti la Uhuru Mkoani Tanga, yeye alihoji uwezekano wa mradi huo kukamilika kwa wakati kwa maelezo kuwa muda uliosalia ni mdogo hadi kufikia kipindi cha mwezi Machi ambao ndiyo matarajio ya mradi kukamilika.
Hofu hiyo ya Mhando iliondolewa na Mhandisi Salum Ngumbi aliyesema kuwa, Mamlaka imejidhatiti kikaamilifu kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwamba vifaa vyote muhimu tayari viko eneo la mradi na kazi zinaendelea huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 45.
Mbonea Herman ni Katibu wa Chama Cha Waandishi wa habari Mkoani Tanga (TPC), alisema kuwa, ziara hiyo ya wanahabari iliyoandaliwa na Tanga UWASA, imeleta maana kubwa katika kuimarisha mahusiano na taasisi hiyo hatua ambayo itasaidia kwenye kufikisha taarifa sahihi kwa umma wa Watanzania.
Mbali na hayo Herman ameelezea kuridhishwa kwake na juhudi zinazoendeshwa na Tanga UWASA, akisema wameonesha jitihada za kujitanua lengo likiwa kufikisha huduma bora kwa wananchi.
Kwa niaba ya wanahabari, Herman aliahidi kuendeleza ushirikiano na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa mazingira Tanga UWASA ili shughuli za utendaji kwenda sawia.
Dkt. Fungo Ali Fungo ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TangaUWASA, katika ziara hiyo hakusita kutoa ya moyoni akisema kuwa, wanahabari wamekuwa na mchango mkubwa katika utendaji kazi wa mamlaka ya Maji Tanga.
Dkt Fungo ametumia jukwaa hilo kuwashukuru waandishi wa habari wa Tanga kwa ushirikiano waliouonesha kwa Tanga UWASA huku akidokeza kuwa, kwa mwaka 2025 Mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ili kuweza kuimarisha na kuboresha hali ya upatikanaji huduma bora kwa wananchi.
Amewasihi Wadau hao wa habari kuendelea na ari ile ile waliyoionesha hapo awali kwa kuwa sehemu ya mabalozi wazuri wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) hatua ambayo itasaidia kuleta tija kwa jamii husika.
Mradi huo wa Hatifungani ya kijani ni matokeo ya jitihada za Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye ubora ambapo Tanga UWASA wamekuja na ubunifu huo katika utendaji wao.
Kwa muda mrefu sasa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Tanga imeendelea kutoa huduma bora kwa Wateja wake huku ikifanya maboresho kwenye miundombinu kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma pasipo changamoto.
Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Tanga (UWASA), Dkt Fungo Ali Fungo akizungumza.Afisa Uhusiano wa UWASA Mkoa wa Tanga,akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo kwa Waandishi wa habari waliotembelea mradi huo.
Muonekano wa mradi huo.
Email: mashakakibaya@gmail.com +255 766 00 33 95.







No comments:
Post a Comment