Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Tanga, Thomas Masese (kulia), akiongoza Viongozi wa wafanyabiashara kukata keki katika hafla fupi kutoa mrejesho utendaji kazi.
...........................................
Na Mashaka Kibaya,Tanga.
KATIKA kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 Mamlaka ya Mapato TRA Mkoani Tanga, imefanikiwa kukusanya shilingi 252.80 bilioni ikivuka lengo la kukusanya bilioni 181.90 kwenye awamu ya kwanza inayoanzia mwezi Julai hadi Disemba 2025 ikiwa ni sawa na asilimia 139.
Katika taarifa yake aliyoitoa Jana kwa Waandishi wa habari ikiwa sehemu ya mrejesho wa utendaji kazi kwa Wadau, Meneja wa TRA Mkoani Tanga, Thomas Masese amesema, hayo ni mafanikio makubwa yaliyopatikana kipindi cha robo ya pili ya mwaka unaoishia mwezi Disemba 2025.
Masese ameeleza kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha kukukua kwa uzalendo na ufanisi wa mifumo ya kodi nchini akisema,walipa kodi wameonesha mwitikio chanya hivyo kuiwezesha TRA kumudu kusanya mapato ya Serikali.
Kwa mujibu wa Masese, ufanisi uliopo katika kukusanya kodi utaiwezesha Serikali kuendelea kutoa huduma zenye ubora kwa wananchi huku akidokeza suala la uimarishwaji wa miundombinu.
Amewashukuru wafanyakazi wa TRA kwa kuonyesha uadilifu katika utendaji kazi wao, huku akiwasihi wadau wengine kuendeleza ushirikiano kwa maslahi ya taifa.
Licha ya kutoa msisitizo katika kuendeleza ushirikiano na kulipa Kodi, Masese amewashauri wafanyabiashara wanaonunua bidhaa nje ya nchi kutumia bandari ya Tanga kwa maelezo kuwa inafanya kazi zake kwa ufanisi.
""Natoa wito wa kuendeleza mshikamano, kutoa elimu kwa walipa kodi ,wanaonunua bidhaa nje ya nchi wanaweza kutumia Bandari ya Tanga hakuna foleni" alisema Masese akiwasihi wadau.
Pamoja na hayo Meneja huyo wa Mamlaka ya Mapato TRA Mkoani Tanga, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wanahabari kwa juhudi za kuendelea kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa maslahi ya Taifa.
Aziza Ramadhani ni Mwenyekiti wa wafanyabiashara wanawake, amepongeza juhudi za TRA kutoa elimu kwa walipakodi hatua ambayo imesaidia wengi kupata TIN tofauti na ilivyokuwa awali.
"TRA ya zamani sio kama ya sasa, tunashirikiana kila mahala, tuendeleze ushirikiano ili mapato ya Serikali yaweze kuongezeke.Wengi tumepata TIN baada ya kuelimishwa"alisema.
Mamlaka ya mapato TRA Mkoa wa Tanga imefanya hafla fupi ya kutoa shukrani na mrejesho wa utendaji wa mwaka uliopita na kuweka ushirikiano na wadau kwa mwaka 2026 ikitambua walipakodi kuwa sehemu ya mafanikio inayojivunia.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato TRA Mkoa wa, Thomas Masese (wa pili kushoto) akizungumza na wafanyabiashara na Wadau wa taasisi mbalimbali.Baadhi ya Wadau wa TRA waliohudhuria hafla fupi iliyoandaliwa na Mamlaka ya mapato kuelekea 2026.
Imeandaliwa na Mashaka Kibaya Email: mashakakibaya@gmail.com
+255 766 00 33 95.







No comments:
Post a Comment