VITONGOJI 527 MKOA WA TANGA KUNUFAIKA NA SH. BILIONI 73.8 ZA MRADI WA UMEME - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, 29 January 2026

VITONGOJI 527 MKOA WA TANGA KUNUFAIKA NA SH. BILIONI 73.8 ZA MRADI WA UMEME

 Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy akizungumza Januari 29, 2026 wakati wa kuwatambulisha Wakandarasi walioshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 527 mkoani Tanga.

..................................

Na Dotto Mwaibale, Tanga. 

VITONGOJI 527 Mkoa wa Tanga vinatarajiwa kunufaika kwa kupata umeme baada Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa zaidi ya Sh.Bilioni 73 kutekeleza mradi wa  kusambaza umeme.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi. Hassan Saidy  aliyasema hayo Januari 29, 2026 Jijini Tanga wakati wa kuwatambulisha Wakandarasi walioshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo kutoka Kampuni ya Giza cable industries pamoja na Energy service Limited. 

 Saidy alisema wamekwisha wapa maagizo wakandarasi hao ya utekelezaji wa mradi huo ambapo wamewataka wawe na timu ya kufanya kazi katika kila wilaya ili kuharakisha kasi ya kuukamilisha.

Alisema wakandarasi hao wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya udhalilishaji kwa  kutoa lugha ambayo itatweza utu wa mtu na rushwa wakati wanatekeleza mradi huo.

 “Unapofanya  kazi ya mradi wa serikali unatakiwa kuwa kama mtumishi wa umma, lugha za kutweza utu wa mtu na kuwarubuni wananchi kwa namna yoyote ile haikubaliki jambo hilo linaweza kusababisha kuvunja mkataba," alisema Mhandisi Saidy.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dadi Kolimba ameipongeza serikali kwa utekelezwaji wa mradi huo na kueleza  kuwa unakwenda kufungua fursa za uchumi vijijini.

“Wakandarasi hawa wawili ambao wametambulishwa leo wanakwenda kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 527 hapa mkoani kwetu ambapo jumla ya Sh. Bilioni 73.8 zimetengwa na Serikali kuptia REA," alisema Kolimba. 

Kolimba alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kuwezesha utekelezaji wa mradi huo na kuwaomba wakandarasi hao kuukamilisha kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mkataba.

Wakati huo huo Kolimba amewaomba wananchi wa maeneo ambayo mradi huo unatekelezwa kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili mradi huo uweze kukamilika na kutimiza malengo ya Serikali pamoja na kuwanufaisha walengwa ambao ni wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi. Hassan Saidy akimkabidhi mkataba Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Dadi Kolimba.
Mmoja wa wakandarasi akizungumza katika tukio hilo la kutambulishwa.
Tukio la kutambulishwa likiendelea.

Taarifa hii imeandikwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990 
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad