BILIONI 200 ZILIZO AHIDIWA NA RAIS SAMIA KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI ZATOLEWA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, 14 February 2026

BILIONI 200 ZILIZO AHIDIWA NA RAIS SAMIA KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI ZATOLEWA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, akizungumza katika Jukwaa la Vijana wa vyuo vikuu na vya kati (Vijana Platform) vilivyopo Mkoa wa Singida 

.............................. 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema kuwa Sh. Bilioni 200  zilizoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na kampuni changa ili wakue kiuchumi zimeaanza kutolewa  na kuagiza zigawiwe  katika wizara za kisekta ili ziweze kuwafikia walengwa.  

Hayo yalibainishwa na Waziri Nanauka, Februari 12, 2026 wakati wa Jukwaa la Vijana wa vyuo vikuu na vya kati (Vijana Platform) vilivyopo Mkoa wa Singida ambalo linawaunganisha vijana makundi mbalimbali wakiwamo wanafunzi, waendesha bodaboda,bajaji,wafanyabiashara wadogo (wamachinga) na vijana waliopo kwenye jamii wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali.

Waziri Nanauka, alitumia nafasi hiyo kuwaagiza viongozi katika mikoa yote nchini kupiga marufuku vijana wanapokwenda kuomba mikopo ya fedha hizo zilizotolewa na Rais Samia kuwaambia hawana sifa za kukopeshwa.  

“Kijana akija ofisini asiambiwe hana sifa bali viongozi hao wamtengeneze ili awe na sifa zitakazomuwezesha kukopesheka na kutumia fursa zilizopo,” alisema Nanauka. 

Alisema Wizara yake ilipewa jukumu la kusimamia na kuratibu fedha hizo ili kuhakikisha vijana wanapewa taarifa na wanapata fursa ya kujua kinachoendelea na utaratibu utakaohusika na kueleza kuwa fedha hizo tayari zimekwisha tolewa na zimeelekezwa katika wizara mbalimbali tayari kwa kutolewa kwa walengwa. 

Alisema baada ya fedha hizo kutoka zimepelekwa katika Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuwakopesha vijana wanaojishughulisha na masuala ya kilimo.
 

Nanauka aliongeza kuwa fedha nyingine zimepelekwa Wizara ya Mifugo na Uvivu kwa ajili ya vijana wanaojishughulisha na uvuvi,wenye vizimba ,wanaotumia maboti  na shughuli zinazoambatana na shughuli hizo. 

Alisema fedha nyingine zimepelekwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa ajili ya vijana wanaojishughulisha na teknolojia, wabunifu wa mambo ya TEHAMA ambapo upo mfuko maalum wa serikali kwa ajili ya watu wenye ubunifu mbalimbali. 

Aliongeza kuwa rais alielekeza katika kipindi cha miaka mitano ni lazima kuwa na kongani la viwanda katika kila wilaya hivyo vijana ambao wanajishughulisha na viwanda vidogo vidogo nao watanufaika na mkopo wa fedha hizo. 

Aidha,aliupongeza mkoa wa Singida kwani katika siku 100 za rais vijana wameweza kukopeswa zaidi ya Sh. milioni. 700 zimetolewa ambazo zinatengwa na halmasauri kila mwezi kutokana na mapato yake ya ndani. 

Kwa upande wake  Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Rasilimali watu, Stephen Pancras, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema mkoa huo unaendelea  na mpango wa kutoa mikopo ya uwezeshaji vijana kupitia halmashauri zake zote za mkoa huo ambazo ni Mkalama, Iramba, Manyoni, Ikungi, Singida DC,Singida MC na Itigi. 

Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 hadi kufikia Januari 20,mwaka huu Mkoa wa Singida umetoa mikopo ya Sh.bilioni 1.4 kwa vikundi 115 kati ya hizo Sh.milioni 733.4 imetolewa kwa vikundi 84 vya vijana vyenye wanachama 429.Vijana wakiwa kwenye jukwaa hiloJukwaa likiendeleaShamra shamra zikiendelea kwenye jukwaa hilo.Waziri Nanauka akiwa na viongozi wengine  kwenye jukwaa hilo. Kulia ni  Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Rasilimali Watu Mkoa wa Singida, Stephen PancrasShamra shamra zikitamalaki kwenye jukwaa hilo.

Habari hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad