Afisa Uchechemuzi, Sera na Mawasiliano wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Florence Majani akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa kongamano la kujadili masuala ya ukatili wa kijinsia na namna ya kukabiliana nayo Januari 23, 2026 mkoani Tanga.
.................................
Na Mashaka Kibaya,Tanga
UKATILI wa Kijinsia ni Vitendo vyote vya Unyanyasaji au Udhalilishaji vinavyofanywa kwa msingi wa jinsia ya mtu, na mara nyingi udhalimu huo umewalenga Wanawake na Watoto.
Kwa nini ukatili wa aina hii huwalenga Wanawake na Watoto? ni kwa sababu ya nafasi zao katika jamii, ukatili huu hujumuisha vipigo, ubakaji, ndoa za utotoni, ukeketaji, manyanyaso ya kisaikolojia, kiuchumi na hata watoto kujikuta wakitelekezwa.
Katika mahojiano na Mwandishi wetu, Jumanne Salmini anasema, mkoani Tanga, ukatili wa kijinsia bado ni changamoto nzito inayochochewa na ukosefu wa elimu, umasikini, mila potofu, na hofu ya wahanga katika suala la kutoa taarifa ili kuweza kusaidiwa.
Anasema, baadhi ya wilaya za mkoa huo, imeibuka tabia kwa baadhi ya wazazi na walezi kuwakataza watoto wao kufaulu mitihani yenye lengo la kuwaruhusu kuendelea na masomo ya juu.
Anasema kwamba, aina hiyo ya ukatili husababushwa na wazazi hao kwa kisingizio cha kukosa uwezo wa kuwaendekeza watoto wao kielimu na hivyo kuwanyima haki ya kupata elimu.
Pamoja na hayo, amesema kuwa watoto wamekuwa wakikumbwa na mimba za utotoni, ukatili wa kingono huku baadhi ya familia zikiendelea kuamini kuwa kumpiga mwanamke au kumuozesha mtoto wa kike mapema ni kawaida.
Kumuozesha mtoto chini ya umri wa miaka 18 bado ni hali inayosababisha mateso makubwa kwa waathirika kwani watoto wengi hukosa sauti ya kujitetea.
Saidi Hemedi kwa upande wake anazungunzia ukatili unaowakumba wanawake akisema, baadhi yao wamekuwa wakilazimika kuvumilia ukatili kwa kuogopa ndoa kuvunjika au kudharauliwa miongoni mwa jamii.
Kiukweli ukatili wa kijinsia una madhara makubwa yaliyo ya muda mrefu kiafya, waathirika hupata majeraha ya mwili, maambukizi ya magonjwa ya zinaa na hata kupatwa na matatizo ya uzazi.
Madhara mengine ni wahusika kuathirika kisaikolojia, msongo wa mawazo, hofu, sonona, kupoteza kujiamini kijamii na kiuchumi, wanawake na watoto hushindwa kushiriki kikamilifu katika elimu na shughuli za maendeleo, hali inayokwamisha ustawi wa familia.
Ili kuweza kukomesha tatizo la ukatili wa kijinsia, ni muhimu kuimarisha elimu kwa jamii kuhusu haki za binadamu, hasa haki za wanawake na watoto huku sheria zilizopo zikiweza kusimamiwa kikamilifu.
Vilevile ushauri umetolewa kwamba wahalifu wanapaswa kuchukuliwa hatua kali bila upendeleo sanjari na vituo vya msaada wa kisheria, kiafya na kisaikolojia kwa waathirika kuboreshwe hadi kuweza kufika ngazi za vijiji.
Wadau wengine wanashauri ushiriki wa viongozi wa dini, wazee wa mila na taasisi za serikali kuona umuhimu katika kubadili mitazamo iliyokuwa potofu.
Jamii ihamasishwe kutoa taarifa za ukatili bila woga, huku watoto na wanawake wakipewa nafasi ya kujieleza. kupitia mshikamano wa jamii, elimu na utekelezaji wa sheria, hapo mkoa wa Tanga utakuwa mfano wa kupambana na kukomesha ukatili wa kijinsia.
Januari 23, 2026 Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kilitolea taarifa utekelezaji wa mradi wa 'Sauti Zetu' unaohusika na kuongeza uelewa, kutoa elimu na kueleza kwa kina ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto.
Mwanahabari Frolence Majani ni Afisa Uchechemuzi, Sera na Mawasiliano wa TAMWA, akiwa Jijini Tanga alisema kutafanyika utekelezaji mradi wa 'Sauti Zetu' unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani GIZ na utakaokuwa wa mwaka mmoja kwa Mikoa mitatu ya Tanzania bara.
Mikoa hiyo ni Tanga kwa wilaya za Kushoto na Tanga Mjini, Dodoma wenye wilaya za Bahi na Chamwino na Dar es Salaam kwa wilaya za Temeke na Kinondoni. Majani alikuwa Jijini Tanga kwa Kongamano la siku moja lililohusisha walimu, wanafunzi, maafisa elimu, vyombo vya ulinzi na usalama na wanahabari wakijadiliana juu ya madhara ya Vitendo vya ukatili wa kijinsia
Katika mradi huo vyombo vya habari vitahusika kuhabarisha umma, kufichua vitendo vya ukatili wa kijinsia, kusudio la mradi likiwa kutoa elimu na kuelezea kwa kina kuhusu ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto ili kuweza kutoa taarifa sahihi kwa waathirika.
Wakati Kongamano hilo likifanyika ilielezwa kuwa, Mkoa wa Tanga umeendelea kuwa eneo lenye kesi nyingi zaidi za vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo wadau waliokutana walitumia jukwaa hilo kujadiliana, kubadilishana uzoefu, kujifunza na kupata taarifa za hali ya ukatili wa kijinsia mkoani humo.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt Rose Reuben ilisema, takwimu za mwaka 2023 kutoka Ofisi ya ustawi wa jamii mkoani Tanga, zinasema, asilimia 33% ya wanawake wamewapitia ukatili wa kijinsia na wa kisaikilojia mwenendo ukioonyesha ongezeko kwenye kasi ya matukio hayo.
Kikanda, takwimu zinaonyesha kuwa kanda ya kaskazini mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha ni yenye kesi nyingi zaidi ya (asilimia 83%) za ukatili wa kijinsia.Wanafunzi wameendelea kuathirika kwa vile, wamekuwa windo la watu wasio na maadili hali ambayo inachangia idadi kubwa kupata mimba na kuacha masomo.
Aidha Wanawake wamekuwa wakipitia madhila makubwa ya unyanyasaji ikiwemo vipigo, matusi na kunyimwa haki zao za msingi, hali ambayo inasababisha kundi hili kuwa katika hali duni kiuchumi, kiafya, kuathirika kisaikilojia na hata wakati mwingine kujeruhiwa.
Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Afisa elimu Msingi, Shomari Bane amekiri kuwepo wa matukio ya ukatili wa kijinsia huku akiwasilisha visa mkasa kadhaa likiwemo tukio la mwanafunzi kuchonwa kisu tumboni akiwa meneo ya shule.
Matukio mengine ya ukatili yaliyobainisha na Bane kwa Tanga ni pamoja na lugha zisizo na stara kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine akieleza kuwa huo nao ni aina mojawapo ya ukatili.
Muendelezo wa taarifa ya TAMWA, imebaini, uwepo wa ombwe kubwa la ukosefu wa taarifa sahihi za matukio ya ukatili, ukosefu elimu juu ya ukatili wa kijinsia, ambapo ni matokeo ya ukosefu wa elimu, mafunzo, vituo jumuishi vya ukatili wa kijinsia, upatikanaji taarifa na ushiriki duni wa wazazi kwenye malezi ya watoto wao.
Mradi wa 'Sauti Zetu' ni matokeo ya jitihada za miaka 39 ya utendaji kazi za kupinga ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto Tanzania bara na Visiwani zinazoendelea kwa kasi huku vyombo vya habari vikiwemo vya 'kidijitali' vikitumika kupaza Sauti ili kutokomeza kabisa ukatili huo.
Umuhimu wa vyombo vya habari kuwa nyenzo muhimu katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto? TAMWA inaamini kuwa, nguvu iliyopo kwenye vyombo vya habari itakuwa chachu ya mafanikio katika kuchunguza, kuibua, kuchangia na kuelimisha juu ya ukatili wa kijinsia na madhara yake kwa jamii nzima.
Imedhihirishwa kuwa, kupitia nguvu iliyopo kwenye vyombo vya habari,TAMWA imekuwa sehemu ya mabadiliko na hatua kubwa ya kupunguza, kufanyiwa kazi Vitendo vya ukatili wa kijinsia ukitolewa mfano mabadiliko ya sheria za ubakaji, sasa mbakaji atahukumiwa kifungo cha maisha jela au kifo.
Mafanikio mengine ni utolewaji wa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya habari,ambapo imeshuhudiwa katika miongo minne ya utendaji kazi,TAMWA pia imetumia vyombo vya habari kuibua matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyochukuliwa hatua na mamlaka husika huku waathirika wakipatiwa haki zao.
Kupitia mradi wa 'Sauti Zetu', TAMWA imeendelea kuziomba mamlaka husika kuendelea kusaidia kupaza sauti kuibua matukio ya ukatili wa kijinsia unaofanyika shule za msingi, sekondari, masokoni na ule wanaofanyiwa wanawake na watoto wakiwa majumbani.
Katika Kongamano hilo TAMWA imetoa wito kwa Ofisi za ustawi wa jamii wilayani Tanga na Lushoto, kuhakikisha zinawapatia taarifa za ukatili wa kijinsia waandishi wa habari ili waweze kuzifanyia kazi.
Aidha waandishi wa habari wameombwa kuendelea kuibua matukio ya ukatili, ulawiti, ukatili wa mtandaoni, vipigo kwa wanawake na watoto na hata udhalilishaji huku wadau wa elimu wakiwemo Wazazi, walimu, walezi wakihamasishwa kuendelea kupaza Sauti kusaidia kufichuliwa kwa matukio ya ukatili wa kijinsia na hivyo kuutokomeza kabisa.
Pia jamii ya watu wa Tanga imetakiwa kutambua kuwa, ukatili wa kutumia mitandao ya 'kidijitali' unaongezeka na hivyo ni wakati wa kuelimishana ili kuweza kumaliza kabisa ukatili huo unaoshika kasi.
Agness Mwafifi Msimamizi miradi kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani 'GIZ', kupitia Kongamano hilo hakusita kuwaasa wadau kutofumbia macho matukio ya ukatili wanayokutana nayo kwenye jamii, akisema kufanya mapato majumbani ni kunapoteza haki.
Mwafifi aliendelea kutumia fursa hiyo ya kuzungumza na walishiriki wa Kongamano hilo akiwasihi, kwa kusema "Kongamano liwe mbegu na chachu ya kuleta mabadiliko katika Mkoani wa Tanga"
Msisitizo umetolewa huku jamii ikihamasishwa kufahamu madhara ya ukatili wa kijinsia, kuelewa namna ya kupata msaada sanjari na wanahabari kutakiwa kutumia kalamu zao vyema katika kufichua ukatili wa kijinsia.
Mradi wa Sauti Zetu unaendeshwa na Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani 'GIZ' unakwenda na Kauli mbiu inayosema" Pamoja tuungane kupinga Ukatili wa Kijinsia ".













No comments:
Post a Comment