MAKAMU WA PILI AFUNGUA SEMINA YA WABUNGE, ASISITIZA UWAJIBIKAJI - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, 26 February 2026

MAKAMU WA PILI AFUNGUA SEMINA YA WABUNGE, ASISITIZA UWAJIBIKAJI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza wakati wa Semina kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar kuhusu Mfuko wa Jimbo, iliyofanyika Zanzibar, Februari 26, 2026, ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu Unguja: 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amefungua semina ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika utekelezaji wa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo.


Semina hiyo imefanyika Unguja, Zanzibar Februari 26, 2026 akieleza kuwa Mfuko wa Jimbo umechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, umeme, elimu, barabara na kukuza shughuli za biashara katika jamii.


Amesema mfuko huo ulianzishwa kwa lengo la kuwashirikisha wananchi katika kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo inayogusa mahitaji halisi ya majimbo yao, hivyo ni wajibu wa wabunge kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu ili miradi iwe na tija na uendelevu.


“Serikali inalenga kuwezesha utekelezaji wa miradi ya haraka yenye manufaa kwa wananchi, kuimarisha uwajibikaji na ushiriki wa jamii katika kupanga na kusimamia maendeleo pamoja na kupunguza pengo la maendeleo kati ya maeneo mbalimbali,” amesema Mhe. Abdulla.


Ameeleza licha ya kuwepo kwa sheria na miongozo ya matumizi ya fedha za mfuko huo, bado kuna changamoto za usimamizi katika baadhi ya halmashauri zilizosababisha kuibuka kwa hoja za ukaguzi. 


Kutokana na changamoto hiyo amewataka watendaji wa halmashauri kusimamia ipasavyo fedha hizo ili kuepuka dosari na kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.


Aidha amezungumzia umuhimu wa kukusanya maoni kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Jimbo ya mwaka 2009, kufuatia maelekezo yaliyotolewa baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa mfuko kwa mwaka 2023/24 katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI.


Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeombwa kuratibu upatikanaji wa maoni kutoka upande wa Zanzibar, hivyo akawahimiza wabunge kutumia semina hiyo kama jukwaa la majadiliano ya wazi na kitaalamu kwa lengo la kuboresha mfumo wa mfuko huo.


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema semina hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha uelewa wa wabunge kuhusu utekelezaji na usimamizi wa Mfuko wa Jimbo.


Amesema maboresho yanayopendekezwa yanalenga kuhakikisha sheria na miongozo ya mfuko inaendana na hali halisi ya utekelezaji na kuongeza uwazi pamoja na ufanisi katika matumizi ya fedha za umma.


Semina hiyo imewakutanisha wabunge kutoka majimbo 50 ya Zanzibar pamoja na viongozi na watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kwa lengo la kujadili kwa kina namna bora ya kuboresha utekelezaji wa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kushoto) akiteta jambo na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kabla ya kufungua Semina kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar kuhusu Mfuko wa Jimbo, iliyofanyika Zanzibar, Februari 26, 2026.

Baadhi ya Wabunge wakiwa kwenye Semina kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar kuhusu Mfuko wa Jimbo, iliyofanyika Zanzibar, Februari 26, 2026, ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati) akimkabidhi zawadi Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla mara baada ya kufungua Semina kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar kuhusu Mfuko wa Jimbo, iliyofanyika Zanzibar, Februari 26, 2026. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Kundi la Vijana Kanda ya Pemba Mhe Zainab Abdallah.
Mbunge wa Kundi la Vijana Kanda ya Pemba Mhe Zainab Abdallah (wa kwanza kushoto) akimkabidhi zawadi Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (kulia) mara baada ya kufungua Semina kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar kuhusu Mfuko wa Jimbo, iliyofanyika Zanzibar, Februari 26, 2026. Wa katikati ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad