Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Geofrey Mdama, akizungumza kwenye kikao cha wadau kilichofanyika hivi kaaribuni mkoaani humo. Kushoto ni Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida, Mhandisi Boniface Shitindi
..........................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limeimarisha mikakati ya kukabiliana na uhujumu wa miundombinu ya umeme kwa kuanzisha doria kali kwa kushirikiana na wananchi kufichua wahalifu, na kutoa zawadi ya kuanzia Sh. 100,000 hadi 1,000,000 kwa watoa taarifa.
Shirika hilo pia limeongeza hatua za kisheria dhidi ya wizi wa nyaya na transfoma ili kulinda miundombinu hiyo.
Katika kukabiliana na vitendo hivyo vya hujuma ya miundombinu ya shirika hilo TANESCO Mkoa wa Singida limewaomba viongozi mbalimbali wa mkoa huo kuanzia madiwani, viongozi wa mitaa na wananchi kushirikiana kukabiliana na vitendo vya hujuma na wizi wa miundombinu ya umeme vinavyofanywa na baadhi ya watu kwa makusudi na kulisababishia shirika hilo hasara.
Ombi hilo limetolewa na Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida, Mhaandisi Boniface Shitindi, wakati akizungumza kwenye kikao cha madiwani,wenyeviti wa mitaa,vijiji na watendaji wa Manispaa ya Singida.
Katika kikao hicho ajenda nyingine iliyozungumzwa ilihusu matumizi ya nishati safi ya kupikia inayotumia umeme kidogo.
Shitindi alisema katika mkoa huo kuna matukio ya wizi wa transfoma pamoja na uharibifu wa miundombinu mingine ya umeme ikiwamo waya wa ulinzi wa radi (earth wire), hali inayohatarisha usalama wa vifaa vya umeme pamoja na kuathiri upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wananchi.
Alisema watu hao wanapoiba ‘Earth Wire’ baada ya kuikata kuiacha transfoma bila ya kuwa na kinga dhidi ya radi, hatua inayosababisha vifaa kuharibika kwa urahisi wakati wa mvua iliyoambatana radi inaponyesha.
Aidha, Shitindi alisema kuwa Mkoa wa Singida unapokea umeme kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu kupitia laini ya msongo wa kilovoti 400, kisha kuusambaza katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini hadi nchi jirani ya Kenya.
Alisema Mkoa wa Singida unapokea megawati 600 huku matumizi yakiwa megawati 27 na kuacha ziada ya megawati 573.
Kufuatia matumizi hayo madogo ya umeme amewaomba wananchi kuacha kutumia mkaa na kuni na badala yake wahamie kwenye matumizi ya nishati safi ya umeme na kueleza kuwa teknolojia mpya za majiko ya umeme zinatumia umeme kidogo na kusaidia kuhifadhi mazingira.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Geofrey Mdama, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, aaaliwaomba wawekezaji wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo kuwekeza katika mkoa huo kutokana na Mkoa wa Singida kuwa na umeme wa kutosha.
Washiriki wa kikao hicho walisema vita dhidi ya wizi wa miundombinu ya umeme vitafanikiwa kwa kushirikiana na shirika hilo na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Geofrey Mdama, akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.









No comments:
Post a Comment