TFS YAANZA MKAKATI WA KUZIBA PENGO LA WATUMISHI, YASISITIZA UWAJIBIKAJI - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 23 February 2026

TFS YAANZA MKAKATI WA KUZIBA PENGO LA WATUMISHI, YASISITIZA UWAJIBIKAJI

MOROGORO: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeanza kutekeleza mkakati maalum wa kuimarisha rasilimali watu ili kukabiliana na upungufu wa watumishi unaoathiri utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi nchini.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Huduma Saidizi, DCC Emmanuel Wilfred Kiboko, amesema Februari 20, 2026 kuwa kwa sasa TFS ina takribani asilimia 48 tu ya watumishi wanaohitajika kulingana na tathmini iliyofanywa kupitia mfumo wa HR-Assessment wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Akizungumza katika siku ya tatu ya Mkutano wa Nne wa Viongozi na Makamanda wa Vituo vya TFS unaoendelea katika Hoteli ya Cate, Morogoro, Kiboko alisema Serikali imetoa vibali vya ajira 862 katika kipindi cha miaka miwili ili kupunguza pengo hilo.

Alisema hadi sasa watumishi 369 wameajiriwa, wamehitimu mafunzo ya kijeshi na kupangiwa vituo vya kazi, huku takribani 300 wakitarajiwa kuanza mafunzo ya urekebu Machi 1, 2026 katika kambi ya Mlele. Aidha, taratibu za ajira kwa wengine zinaendelea kukamilishwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

“Hatua hizi zitasaidia kupunguza pengo la watumishi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za misitu,” alisema.

Tathmini ya utendaji

Kiboko alisisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia utekelezaji wa Mfumo wa Tathmini ya Utendaji Kazi (PEPMS), akibainisha kuwa nyongeza ya mshahara ya kila mwaka sasa inategemea moja kwa moja kiwango cha utendaji wa mtumishi.

Aliwataka makamanda kusimamia kikamilifu matumizi ya mfumo wa e-Utendaji ili kuimarisha uwajibikaji na tija katika taasisi.

Uwajibikaji na maadili

Katika hotuba yake, Kiboko alikumbusha kuwa pamoja na juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya kazi, watumishi wanapaswa kuzingatia nidhamu, uadilifu na weledi kazini.

“Serikali imeshatimiza wajibu wake. Sasa ni jukumu letu kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma,” alisema, akionya kuwa hatua stahiki zitachukuliwa kwa watakaokiuka taratibu.

Ikama na bajeti

Kuhusu mipango ya baadaye, alisema maandalizi ya ikama na bajeti ya mwaka 2026/27 yamekamilika, yakilenga kuoanisha mahitaji ya watumishi na majukumu ya wakala katika kusimamia misitu ya Tanzania Bara.

Mkutano huo unaendelea kujadili mikakati ya kuimarisha utendaji, kuongeza ufanisi wa askari na maafisa wa uhifadhi, pamoja na kuimarisha misingi ya “Kazi na Utu” katika utoaji wa huduma kwa umma.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad