WAKAZI MGEULE WALIA KUWEKEWA ALAMA YA X NYUMBA ZAO - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, 8 February 2026

WAKAZI MGEULE WALIA KUWEKEWA ALAMA YA X NYUMBA ZAO

 

 Elizabeth Mwakapangala akionesha hukumu aliyoshinda kesi ya ardhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

.............................. 

Na Mwandishi Wetu.          

WAKAZI wa Mgeule, Kata ya Buyuni, Ilala, jijini Dar es Salaam,  wamemlilia Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kinyamwezi, Fahad Mlali akidaiwa kuweka alama ya X katika nyumba zao, bila kufuata taratibu za kisheria.     

Wakizungumza jijini katika eneo hilo la Mgeule, baadhi ya wakazi hao walishangaa nyumba zao kuwekewa alama hizo,  wakati ni mwenyekiti wa mtaa mwingine.

Mmoja wa wakazi hao, Ikram Idd alisema anashangaa nyumba yake kuwekewa X wakati alinunua kihalali kutoka kwa Elizabeth Mwakapangala. 

 Idd alisema kitendo cha mwenyekiti huyo kuwawekea alama hizo ni kinyume cha sheria, lakini pia si mwenyekiti wa mtaa huo.

Alisema wao ni wakazi wa Mgeule, katika Kata ya Buyuni, lakini anashangaa kuona mwenyekiti huyo kwenda kufanya tukio hilo katika mtaa unaongozwa na mwenyekiti John Mwaitebele.  

Naye, Aisha Ramadhan alisema kitendo cha mwenyekiti wa Kinyamwezi kumwekea X katika nyumba yake ni uvunjifu wa amani. 

Aisha aliiomba serikali ngazi ya juu  kuingia kati suala hilo, kwani linatishia amani kwa wakazi wa eneo hilo. 

Pia alisema alinunua eneo  kihali na hapakuwepo na mgogoro wa ardhi, lakini baada ya kujenga amejitokeza mwenyekiti wa Kinyamwezi kudai lipo upande wake. 

Kwa upande wake, Elizabeth ambaye aliwauzia viwanja wakazi hao alisema eneo hilo ni mali yake baada ya kushinda kesi katika Mahakama Kuu ya. Ardhi Tanzania. 

Awali Elizabeth  alifungua kesi ya ardhi katika mahakama hiyo iliyomshtaki Mkurugenzi wa Manipaa ya Ilala na Mamlaka ya Viwanja vya Needy kwa kutwaa eneo lake bila kufuata sheria, baadaye alishinda kesi hiyo.

Alisema baada ya kushinda kesi hiyo anashangaa kuona mwenyekiti wa Kinyamwezi anatuma watu kuja kuzika katika hilo, lakini akiweka alama ya X katika nyumba za wakazi wa eneo hilo bila kufuata utaratibu kwa mujibu wa sheria.

Alisema madai ya mwenyekiti huyo anawataka wakazi wa Kinyamwezi waendelee kuzika katika eneo hilo, licha ya mahakama kumpa haki baada ya kushinda kesi.  

Mjumbe wa shina namba moja wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Hamad Makame, alisema mgogoro wa eneo hilo ulimalizika kabla ya mwenyekiti wa sasa wa mtaa wa Kinyamwezi  kuingia madarakani mwaka juzi.

Makame alisema eneo hilo, lipo katika mtaa wa Mgeule na mpaka ni mto nyamalonda.                      Alisema anashangaa kuona mwenyekiti wa Kinyamwezi anafika kuweka X katika nyumba  za watu kinyume cha sheria.  

Makame aliongeza kuwa akiwa mjumbe wa shina katika eneo hilo hajapata barua yoyote kutoka katika mamlaka husika ya kumruhusu mwenyekiti huyo kuweka X kwenye nyumba za watu, lakini kuwaruhusu watu kuzika katika eneo la mtu. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kinyamwezi, aliyetajwa kwa jina la Fahad  Mlali amekiri kwenda kuweka alama hizo akidai eneo hilo ramani yake inasomeka lipo Kinyamwezi na aliojenga hapo ni wavamizi.  

Mlali alisema alihitaji wakazi wa eneo hilo waondoke ili liweze kutumika kwa kuzikia. Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgeule, John Mwaitebele alisema eneo hilo ni halali la Elizabeth baada ya kuishtaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Mkurugenzi wa Manipaa ya Ilala na kushinda kesi. 

Mwaitebele huyo alisema kutokana na suala hilo, vitendo vinavyoendelea katika eneo hilo ni ukiukwaji wa sheria.   

Wakazi wa Mgeule wakionesha alama ya X zinazodaiwa kuwekwa na Mwenyekiti wa Kinyamwezi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad