Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati kuu ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Iikiongozwa na Mwenyekiti ya JMAT Dkt.Alhad Mussa Salum, Mchungaji George Fupe, Sheikh Twalib Ahmad, Askofu Charles Howard pamoja na Balozi Fatma Kikkedes walipokutana Tarehe 19 Februari 2026 Makao makuu ya JMAT Mkoani Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Dkt. Alhad Mussa Salum Akimkabidhi Katiba ya Jumuiya hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu mbele ya wajumbe wa Kikao maalum cha Wizara na Jumuiya hiyo kwa lengo la wizara kujitambulisha na kujadiliana na wadau wa Mahusiano Tarehe 19 Februari 2026 Mkoani Dar es salaam katika Ofisi za Makao Makuu ya JMAT.
-----------------------------------------
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Clement Sangu (Mb.) ametembelea Ofisi za Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Makao Makuu Februari 19 2026 Jijini Dar es Salaam na kukutana na Viongozi kwa lengo la kujitambulisha na kulitambulisha jukumu jipya la Mahusiano ambalo Ofisi yake imekabidhiwa kuliratibu.
Aidha, Waziri Sangu alipowasili amepokelewa na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT ) Dkt. Alhad Mussa Salum pamoja na wajumbe wa jumuiya hio.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Sangu alipongeza Jumuiya hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano nchini kupitia Maridhiano.
Vilevile, alieleza kuwa JMAT imekuwa nguzo muhimu ya maadili na mshikamano wa kijamii kwa kuhimiza maridhiano ya amani, kuvumiliana na kuimarisha mahusiano mema baina ya waumini wa dini mbalimbali.
"Juhudi hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa kudumisha utulivu na mshikamano wa kitaifa" amesema Mhe. Sangu.
Aidha, Mhe. Sangu amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kidini katika kushughulikia changamoto za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kikanda na kimataifa hususan malezi bora na maadili mema katika jamii.
Sambamba na hayo, ameihakikishia JMAT kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na Baraza hilo na taasisi mbalimbali kuendeleza agenda ya amani, mshikamano na maendeleo jumuishi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Dkt. Alhad Mussa Salum, amempongeza Rais kwa kutambua umuhimu wa Mahusiano na kuanzisha Wizara mahsusi inayoshughulikia mahusiano.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa kutambua na kuthamini mchango wa Jumuiya na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha umoja wa kitaifa, amani na mshikamano.











No comments:
Post a Comment