Na Mwandishi wetu - Kilimanjaro
Kamati ya Mpango wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika wilaya za Mwanga na Same, mkoani Kilimanjaro, zimekutana kujadili mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kujitokeza katika jamii, huku zikisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanaume katika juhudi za kukomesha vitendo hivyo.
Mkutano huo ulioandaliwa na TGNP Mtandao uliwakutanisha wajumbe wa kamati za MTAKUWWA, watu mashuhuri kutoka katika jamii pamoja na wataalamu kutoka Vituo vya Taarifa na Maarifa (KC).
Pamoja na mambo mengine, washiriki walijadili pia namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kuathiri maisha ya wananchi na kuchangia changamoto za kijamii ikiwemo ukatili wa kijinsia.
Akizungumza katika mkutano huo, mwezeshaji Dkt. Katanta Simwanza alisema mpango huo unalenga kuongeza uelewa kwa jamii, hususan wanawake, ili kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuimarisha ushiriki wao katika uongozi na utoaji wa maamuzi katika ngazi mbalimbali za jamii.
Alisema licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa, changamoto ya ukatili wa kijinsia bado inaonekana katika baadhi ya maeneo ya wilaya hizo, ambapo vitendo kama vipigo kwa wanawake na ushiriki mdogo wa wanawake katika maamuzi ya kifamilia na kijamii vinaendelea kujitokeza.
Aidha, wajumbe wa mkutano huo walijadili umuhimu wa kuwepo kwa mifumo itakayowahusisha wanaume zaidi katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku baadhi yao wakieleza kuwa wakati mwingine wanaume wamekuwa wakihisi hawashirikishwi ipasavyo katika kutatua changamoto zinazohusu familia na jamii.
Washiriki wa mkutano huo walisema vitendo vya ukatili wa kijinsia vina athari nyingi katika jamii, ikiwemo matatizo ya kiafya, migogoro ya kifamilia na kupungua kwa ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo.
Mchungaji Rafaeli Mbwambo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, alisema mifumo kandamizi iliyojengeka kwa muda mrefu katika jamii imechangia wanawake kukosa nafasi ya kutoa maoni yao katika maamuzi ya familia na jamii.
“Nimeona jinsi mifumo kandamizi ilivyochukua nafasi katika jamii yetu, ambapo wanawake walionekana kama hawana sauti huku wanaume wakionekana kuwa na mamlaka ya maamuzi. Ingawa hayakuandikwa rasmi, mifumo hiyo imejengeka katika maisha ya jamii kwa muda mrefu,” alisema.
Kwa upande wake, Yuda Mziray kutoka wilaya ya Same alisema mafunzo aliyoyapata kupitia mpango huo yamebadilisha mtazamo wake kuhusu mgawanyo wa majukumu ndani ya familia.
Naye Hadija Msuya, mjumbe wa Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Lembeni wilayani Mwanga, alisema bado kuna matukio ya vipigo kwa wanawake katika baadhi ya maeneo, lakini kwa sasa waathirika wameanza kutoa taarifa kupitia vituo hivyo ili kupata msaada.
Alisema elimu inayoendelea kutolewa kwa jamii imeanza kuongeza uelewa kuhusu haki za wanawake na umuhimu wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake, Imamu wa Msikiti wa Kisangara wilayani Mwanga, Omari Abdi Msofe, alisema viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu haki za binadamu na umuhimu wa kupinga ukatili wa kijinsia.
Washiriki wa mkutano huo walisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, huku wakiiomba serikali kuendelea kutoa kipaumbele kwa masuala ya wanawake ili kuhakikisha kunakuwepo usawa katika maendeleo ya jamii.









No comments:
Post a Comment