MGONJWA ALIYEDAIWA KUZUILIWA KWA DENI HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA AAGWA DAR, KUZIKWA MANYARA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 23 March 2026

MGONJWA ALIYEDAIWA KUZUILIWA KWA DENI HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA AAGWA DAR, KUZIKWA MANYARA

Ndugu zake wa marehemu Ester John Furaha wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mpendwa wao wakiliingiza kwenye Hiace tayari kwa safari ya kwenda nyumbani kwao Kijiji cha Bashanga Kata ya Waleta Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara kwa maziko yake yatakayofanyika kesho Machi 24, 2026.

.................................

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam


MGONJWA Ester John Furaha (32), ambaye alipewa rufaa kwenda Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu baada ya kudaiwa kuzuiliwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa deni la Sh.1,175,000, ameagwa rasmi huku ndugu, jamaa na marafiki wakieleza masikitiko yao makubwa kufuatia kifo chake. 


Mwili wa marehemu Ester uliagwa leo Machi 23, 2026 majira ya saa 12 jioni katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, ambapo baadhi ya ndugu zake wa karibu pamoja na watu walioguswa na tukio hilo walihudhuria kutoa heshima za mwisho. 


Katika hafla hiyo fupi ya kuuaga mwili, hali ya huzuni ilitawala huku wengi wakishindwa kujizuia kumwaga machozi wakikumbuka mateso aliyopitia marehemu kabla ya kifo chake. 


Akizungumza kwa niaba ya familia, mdogo wa marehemu, Celina Furaha, aliwashukuru watu wote waliotoa msaada wa hali na mali hadi kufanikisha kusafirishwa kwa mwili wa dada yake kwenda nyumbani kwao kwa ajili ya maziko. 


Alisema familia inathamini mchango wa kila mmoja aliyejitokeza kuwafariji katika kipindi kigumu walichopitia.


“Tunawashukuru sana wote walioguswa na msiba huu, kuanzia waliotusaidia gharama za matibabu, usafiri wa mwili hadi waliotufariji kwa maneno. Mungu awabariki sana,” alisema Celina kwa sauti ya huzuni. 


Kwa mujibu wa familia, maziko ya marehemu yanatarajiwa kufanyika kimila kesho Machi 24, 2026 katika Kijiji cha Bashanga, Kata ya Waleta, Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara, ambako ndugu na wanakijiji wanatarajiwa kushiriki kumpumzisha katika nyumba yake ya milele.


Baadhi ya waombolezaji waliohudhuria walisema kifo cha Ester ni pigo kubwa kwa familia na jamii, wakimtaja kuwa mtu mwenye upendo, uvumilivu na aliyepigana hadi dakika za mwisho kutafuta nafuu ya afya yake licha ya changamoto alizokutana nazo.


Katika salamu zao za rambirambi, ndugu na marafiki walitoa ujumbe wa mwisho wakisema: “Buriani Ester John Furaha, mwendo umeumaliza kwa mateso makali. Nenda kapumzike kwa amani. Mungu akupe pumziko la milele. Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.” 

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale Simu: 0754362990

Jeneza lenye mwili wa Ester likitolewa Chumba cha kuhifadhi maiti katika Taasisi ya Saratani Ocean Road tayari kwa safari ya kwenda nyumbani kwao kwa mazishi.
Mmoja wa ndugu wa marehemu akimfariji mdogo wa marehemu Celina Furaha ambaye usiku na  mchana na katika mazingira magumu alipambania uhai wa dada yake kwa kumsaidia alipolazwa kwa matibabu katika hospitali mbalimbali hadi alipofariki.
Ndugu na jamaa wa Ester wakiwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam wakisubiri kuchukua mwili wa mpendwa wao Ester.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad