..................................
Na Dotto Maibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Halima Dendego amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita mkoa huo ulipokea Sh. 1.7 trilioni kwa ajili ya mipango ya maendeleo na usimamizi wa shughuli za Serikali.
Dendego aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha kamati ya ushauri Mkoa wa Singida kilichoketi Machi 8, 2026 mkoani humo.
‘’ Katika kipindi cha miaka minne mkoa wetu umepokea kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo na usimamizi wa shughuli za Serikali tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkk. Samia Suruhu Hassan kwa kutupatia fedha hizo,’’ alisema Dendego.
Dendegu alisema Mkoa wa Sngida umeendelea kuwa na utulivu mkubwa kijamii na kisiasa na umeendelea kuwa salama na usalama mkubwa wa chakula kutokana na uzalishaji mkubwa unaofanywa na wananchi.
‘’ Na hata sasa Baraka za mvua zimeendelea kuneemesha mazao yetu mashambani hivyo tunakila sababu ya kumshukuru Mungu kwa Baraka hii kwani yapo maeneo hadi sasa mvua imekuwa kitendawili kikubwa,’’ alisema Dendego.
Alisema wote tumeshuhudia jinsi Serikali inavyoshirikiana na sekta binafsi, washirika wa maendeleo kwa kufanya vizuri sana kwenye mambo mengi yasiyotarajiwa kama vile kumpata Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigule Nchemba, Naibu Waziri-OR-Mipango na Uwekezaji Dkt. Pius Chaya na Balozi na Mshauri wa Rais –Diplomasia Mhe. Dkt. Lazaro Nyalandu.
Alitaja mambo mengine makubwa yasiyotarajiwa ni mkoa kumpata mwakilishi wa Bnge la Dunia Elibariki Kingu, mwakilishi wa Bunge la Afrika Mhe. Asha Feruzi na Maadhimisho ya Kitaifa ya Mei Mosi yaliyofana, kupokea Kombe la CECAFA kupitia timu yetu ya Singida Black Stars pamoja Mamlaka ya Mapato Tanzania '' TRA' kupata TUZO ya mkusanyaji bora wa mapato.
Aidha, Dendego alisema wastani wa pato la mkoa limeendelea kuongezeka japo si kwa kasi inayotakiwa na kwa sasa limefikia Sh. Trilioni 3.196 kutoka Sh.trilioni 2.700.
Alisema kwa wastani wa pato la mwananchi mmoja mmoja pia limeendelea kuongezeka kwa kufikia wastani wa Sh. 1,790,704 mwaka 2024/ 2025 kutoka Sh.1,588,605 mwaka 2020/ 2021 na kueleza kuwa pato hilo ni dogo ukilinganisha na malengo ya Serikali kwenye Dira 2050.
Dendego aliongeza kuwa Mkoa wa Singida umeendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato kupitia TRA na Mapato ya ndani ya Halmashauri.







No comments:
Post a Comment