MWALIMU ALIYETESEKA KWA KISUKARI MIAKA 17 AFARIKI HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA DODOMA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, 28 March 2026

MWALIMU ALIYETESEKA KWA KISUKARI MIAKA 17 AFARIKI HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA DODOMA

Ni Helena Nyahuru Mahamba
Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba alipokuwa akipigania uhai wake wakati akiumwa.
Mwalimu Helena Mahamba, alivyokuwa enzi ya uhai wake.

....................................... 

Na Dotto Mwaibale, Dodoma

MWALIMU Helena Mahamba wa Shule ya Msingi Unyakhae katika Manispaa ya Singida ambaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa miaka 17 amefariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mahamba ambaye alikuwa amelazwa ghorofa ya pili chumba namba mbili katika hosptali hiyo amefariki Machi 28, 2026 saa 9 usiku.

Helena Mahamba baada ya kushindwa kumudu gharama za matibabu alilazimika kubaki nyumbani akijiuguza huku hali yake ikiendelea kudhoofu kila siku.

 Taarifa zake zilipotolewa kwenye mitandao ya kijamii akiomba msaada wa matibabu na kwa jitihada za Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi alipoisoma taarifa hiyo aliagiza mgojwa huyo apelekwe Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kuanza matibabu upya mara moja.

Pamoja na kuanza matibabu hali yake iliendelea kuwa mbaya na Machi 14, alipata rufaa ya kuhamishiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kwa ajili ya kuendelea kupata matibabu.

Mwalimu Mahamba wakati akipigania uhai wake akiwa nyumbani kwake eneo la Unyakhae alidai kuwa tangu alipokuwa anaumwa katika kipindi cha miaka 17 Chama cha Walimu Tanzania  (CWT) Manispaa ya Singida kama mwana chama wao kilimpatia Sh. 100,000 tu huku mwajiri wake naye akishindwa kumsaidia.

Baadhi ya viongozi wa chama hicho wakielezea suala hilo walisema katika katiba yao hakuna kipengele ambacho kinaeleza mwanachama wao anapokuwa na changamoto yoyote ikiwemo kuumwa apatiwe msaada na kama atapatiwa ni msaada tu wa vitu vidogo vidogo kama matunda ambavyo atapatiwa kama hisani.

Kauli hiyo iliwaibua baadhi ya walimu na  kuomba katika katiba yao kuwepo kipengele cha kuwasaidia walimu wanapo kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kuumwa  kutokana na michango yao wanayoichangia kila mwezi.

Mmoja wa Walimu hao Robert Mtinga alisema katika Manispaa ya Singida wapo  zaidi ya 800 na kila mwezi kila mmoja  hukatwa siyo chini ya Sh. 33,000 na wale ambao wapo daraja la juu hukatwa zaidi ya kiwango hicho na kueleza kuwa ni fedha nyingi zinazokusanywa.

Aliongeza kueleza kuwa yakipigwa mahesabu ni fedha nyingi ambazo zinapatikana katika manispaa hiyo ambapo wanaomba ziwe zinatumika kuwasaidia wanapokuwa na changamoto badala ya kusubiri kusaidiwa jeneza na kusafirishwa kwenda makwao wakifariki.

Kwa upande wake Mwalimu Helman Magoti alisema ni vema kuipitia katiba yao vizuri ili kuielewa kama hakuna kipengele cha kutambuliwa wanapokuwa na changamoto ya maradhi ili wapiganie kiwekwe kwa maslahi mapana ya walimu.

Mama wa marehemu Helena, Regina Mahamba ambaye alikuwa akimuuguza amesema licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na wauguzi pamoja na madaktari wa hospitali hiyo katika kumtibu binti yake hali ilibadilika na Machi 28, 2026 alifariki.

Mama Mahamba amesema taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwao Mkuhungu Chama jijini Dodoma.

Buriani Mwalimu Helena Mahamba mwendo umeumaliza kwa mateso makubwa, kapumzike kwa amani huku ukiwaachia walimu wenzako changamoto ya kupigania haki na maslahi yao kwa mwajiri na CWT.

Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa jina lake Lihimidiwe Milele Daima.

Taarifa hii imeandikwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad