Mwalimu Helena Mahamba (42), mkazi wa Unyakhae Manispaa ya Singida alivyo hivi sasa akipambania uhai wake,
.....................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
Mwalimu Helena Mahamba (42), mkazi wa Unyakhae katika Manispaa ya Singida, anaendelea kupambana na hali mbaya ya afya kutokana na ugonjwa wa kisukari unaomsumbua kwa zaidi ya miaka 17, hali inayomlazimu kuwaomba Watanzania kujitokeza kumsaidia gharama za matibabu.
Mwalimu huyo anaishi kwa kutegemea sindano za insulin kila siku baada ya kongosho lake kushindwa kufanya kazi. Kutokana na hali hiyo, amekuwa akitumia muda mwingi akiwa amelala huku akisumbuliwa na maumivu makali ya viungo, kuvimba miguu na mwili mzima, jambo linalomfanya ashindwe hata kutembea.
“Naomba msaada wananchi wenzangu, ugonjwa wa sukari unanisumbua sana. Imefika wakati sitoki ndani, miguu inavimba na mwili mzima. Licha ya kuwa na bima ya afya, sipati dawa zote ninazohitaji hivyo nalazimika kununua mwenyewe,” alisema Mahamba kwa huzuni.
Alieleza kuwa kuna wakati hali yake ilizidi kuwa mbaya na kulazimika kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), ambapo alikuwa akitakiwa kulipa Sh.100,000 kwa siku, gharama ambazo hakuweza kuzimudu.
Amesema changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa ni ukosefu wa fedha za matibabu na lishe maalum anayohitaji kama mgonjwa wa kisukari.
Mahamba, ambaye alianza kuugua mwaka 2010, amesema kwa sasa anaishi kwa kujidunga sindano mbili za insulin kila siku, hali inayomchosha na kumfanya apoteze hamu ya kula na hata ya kuendelea na maisha ya kawaida.
“Naombeni msaada Watanzania wenzangu, nishikeni mkono kwa chochote mtakachojaliwa na Mwenyezi Mungu. Ni kweli mimi ni mwalimu, lakini imefika mahali nimeishiwa kila kitu. Ndugu zangu nao wamechoka kunisaidia kutokana na kuumwa kwa muda mrefu,” alisema Mahambe huku akitokwa na machozi.
Mwalimu Mahamba ana watoto wawili anaowalea, huku akidai kupata msaada mdogo kutoka kwa mtalaka wake anayeishi Dodoma pamoja na familia yake mpya.
Kwa upande wa mwajiri wake, Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Mahamba alisema Mwalimu Mkuu wa shule anapofundisha, Betrida Felician, aliandika barua ya kumuombea msaada wa matibabu miezi mitatu iliyopita. Hata hivyo, alipofuatilia hivi karibuni alielezwa kuwa ombi lake bado lipo kwenye mchakato.
Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Felician alisema mwajiri wao anaifahamu changamoto ya Mahamba na kwamba wamekuwa wakimsaidia kwa kadri ya uwezo wao huku wakisubiri majibu ya maombi ya msaada wa matibabu.
“Suala hili linafahamika, lakini limechukua muda mrefu kwa sababu wagonjwa wanaohitaji kusaidiwa ni wengi. Tunawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia,” alisema Felician.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Moses Msai, alikiri kufahamu changamoto hiyo na kusema wamekuwa wakimtembelea kumjulia hali na kwamba atafuatilia kwa mwajiri kuona hatua iliyofikiwa kuhusu ombi lake.
“Sisi hatuna mfuko maalum wa kuchangia, lakini panapotokea changamoto kama hii huwa tunakwenda kumtembelea na kutoa msaada kadri ya uwezo. Tumeshawahi kumtembelea mara mbili,” alisema Msai.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa katika kipindi chote cha miaka 17 tangu aanze kuugua, chama hicho kimemtembelea mara mbili na kumpatia jumla ya Sh.100,000 tu, mara ya kwanza Sh.50,000 na mara ya pili tena alipokuwa amelazwa ICU mwishoni mwa mwaka jana.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe.Yagi Kiaratu alipopigiwa simu mara kadhaa kwa lengo la kuona namna gani watamsaidia mwalimu huyo alikata simu na kutuma ujumbe mfupi kuwa alikuwa kwenye sherehe.
Jitihada za kumpata mtalaka wa mwalimu huyo aliyetajwa kwa jina la Waelo Manamba ambaye anadaiwa ni Askari Polisi mkoani Dodoma zinaendelea kufanyika ili kujua anamsaidieje mzazi mwenzake huyo anayepitia wakati mgumu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Bi Joanfaith Kataraia alipopigiwa simu jana Machi 4, 2026 alisema hajui chochote kuhusu kuumwa kwa mwalimu huyo.
“ Sijui chochote kuhusu kuumwa kwa mwalimu huyo ndiyo kwanza unaniambia. Maadamu nimepata taarifa nitalifanyia kazi jambo hilo, kesho nikiwa ofisini nitawatuma wasaidizi wangu wakamuone leo nipo kwenye sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake, “ alisema Katarai.
Kwa sasa, Mwalimu Helena Mahamba anahitaji msaada wa haraka wa fedha kwa ajili ya matibabu, ununuzi wa dawa na lishe maalum. Watanzania, taasisi za Serikali, sekta binafsi, wafanyabiashara na watu binafsi wanahimizwa kujitokeza kumsaidia ili kuokoa maisha yake.
Kwa yeyote atakayeguswa kumsaidia, anaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0787 820053 au 0759 521565. Pia anaweza kutuma mchango kupitia Akaunti Namba 0152364578800, Benki ya CRDB, kwa jina la Helena Nyahuru Mahamba.
Mwenyezi Mungu awabariki wote watakaoguswa kumsaidia, kwani mchango wowote, mkubwa au mdogo, utakuwa faraja na msaada mkubwa kwake katika kipindi hiki kigumu cha maisha yake.







No comments:
Post a Comment