MIPANGO YA KULIWEKA SAFI JIJI LA DODOMA YAWEKWA WAZI, BILIONI 3 ZATENGWA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, 3 April 2026

MIPANGO YA KULIWEKA SAFI JIJI LA DODOMA YAWEKWA WAZI, BILIONI 3 ZATENGWA

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, akizungumza na wanahabari (hawapo pichani)

..................................
 

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeweka wazi mipango mbalimbali ya kuboresha usafi wa mazingira jijini humo, ikiwemo kutumia mfumo wa kukodisha huduma kwa sekta binafsi (outsourcing), matumizi ya teknolojia na utekelezaji wa miradi ya muda mrefu. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, jiji hilo limetenga Shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa taka na kuhakikisha Dodoma inakuwa miongoni mwa majiji safi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 2, 2026, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, alisema fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani ya halmashauri, jambo linaloonesha uwezo wa jiji kujitegemea katika kugharamia miradi ya maendeleo.

“Suala la usafi wa mazingira halikwepeki. Tunataka kuwa na jiji safi wakati wote, ndiyo maana katika bajeti yetu mpya tumetenga takribani Shilingi bilioni tatu ili kuhakikisha vifaa vyote vya kukusanyia taka vinapatikana,” alisema Chaula.

Alifafanua kuwa sehemu ya fedha hizo itatumika kusambaza madastbini makubwa katika maeneo mbalimbali ya jiji, yenye mfumo wa utenganishaji wa taka. Hatua hiyo inalenga kurahisisha ukusanyaji, usafirishaji na uchakataji wa taka pamoja na kulinda afya za wananchi.

“Mkakati wetu ni kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi muda wote. Hili linawezekana kwa kuweka miundombinu bora na kwa kushirikiana na wananchi,” alisisitiza.

Mfumo wa Kukodisha Huduma kwa Sekta Binafsi

Tangu mwaka 2018, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilianza rasmi kutumia mfumo wa kukodisha makampuni binafsi kusimamia ukusanyaji na usafirishaji wa taka ngumu. Kupitia mfumo huo, kampuni mbalimbali zimepewa mikataba ya kuhudumia maeneo tofauti ya jiji.

Miongoni mwa kampuni hizo ni Green Waste Pro, ambayo inasimamia ukusanyaji wa taka katika kata nane za katikati ya jiji, zikiwemo Majengo, Kilimani, Madukani na Makole. Maeneo hayo yalichaguliwa kutokana na kuzalisha kiasi kikubwa cha taka na kuwa na idadi kubwa ya taasisi pamoja na wafanyabiashara.

Katika utekelezaji wake, taka huzolewa mara mbili kwa wiki katika maeneo mengi ya makazi, huku masoko na maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa taka yakihudumiwa kila siku. Aidha, mfumo huo umeambatana na matumizi ya vifaa vya kisasa kama magari yenye brashi kwa ajili ya kufagia barabara na mitaa.

Kabla ya mwaka 2018, huduma hizo zilikuwa zikitolewa na mashirika ya kijamii (CBOs), lakini kuanzishwa kwa mfumo wa outsourcing kumeongeza ufanisi na kuboresha kiwango cha usafi jijini.

Mpango wa Maendeleo Endelevu

Jiji la Dodoma pia limeandaa mpango wa muda mrefu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa lengo la kuifanya Dodoma kuwa jiji linalokalika ifikapo mwaka 2050.

Miongoni mwa mikakati iliyopo ni kuhimiza utenganishaji wa taka kuanzia majumbani, ambapo wananchi watatakiwa kutenganisha taka zinazooza na zisizooza kabla ya kukusanywa. Vilevile, jiji linaandaa mfumo wa kidijitali wa kukusanya ada za usafi ili kuongeza ufanisi wa mapato.

Pia kuna mradi wa majaribio wa kuzalisha nishati ya biogas kutoka taka za chakula, hatua inayotarajiwa kupunguza kiasi cha taka zinazopelekwa dampo na kuchangia uzalishaji wa nishati mbadala.

Usimamizi wa Maji Taka

Katika upande wa usimamizi wa maji taka, mamlaka ya DUWASA inaendelea kupanua mtandao wa mabomba ya maji taka, huku mfumo wa sasa ukitumia mabwawa ya kusafishia maji taka yaliyopo eneo la Swaswa. Mipango ipo ya kujenga mabwawa makubwa zaidi na ya kisasa mbali na makazi ya watu ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya wakazi.

Maendeleo ya Miundombinu

Kupitia mpango wa Sustainable Dodoma Vision 2025, juhudi zinaendelea kuboresha mifumo ya mifereji ya maji ili kuzuia mafuriko na uchafu mitaani. Aidha, jiji linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira na kuhimiza uwekezaji katika viwanda vya urejelezaji wa taka kama plastiki, vioo na vitambaa.

Kwa mujibu wa tathmini ya jiji, utekelezaji wa mfumo wa outsourcing tangu mwaka 2018 umeongeza kiwango cha usafi, huku zaidi ya asilimia 64 ya wakazi wakiridhishwa na hali ya sasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Meya Chaula aliwataka wananchi kuendelea kulipa kodi kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo usafi wa jiji, akisisitiza kuwa mchango wa wananchi ni msingi wa maboresho ya huduma.

Mpango huo unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa taka na kulifanya Jiji la Dodoma kuwa safi, salama na linalovutia  wakazi pamoja na wageni mbalimbali watakaotembelea jiji hilo..

Makala hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad