Rais wa Uganda,
Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais
mstaafu wa Tanzania na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kwa Ukanda wa
Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, katika Ikulu
ndogo ya Nakasero jijini Kampala, Jumanne tarehe 7 Aprili 2027.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili walijadili hali ya kisiasa na
kiusalama nchini Sudan Kusini, wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya amani na
maridhiano kati ya pande husika ili kurejesha utulivu wa kudumu.
Rais Museveni alimweleza Dkt. Kikwete kuwa Uganda itaendelea kuunga mkono
juhudi zote za kuleta amani nchini humo, akibainisha kuwa utulivu wa Sudan
Kusini, hasa katika eneo la Equatoria ambako kuna idadi kubwa ya raia wa
Uganda, ni muhimu kwa usalama wa kikanda na ustawi wa kiuchumi.
Dkt. Kikwete, mwenye uzoefu mkubwa wa kidiplomasia katika masuala ya amani barani Afrika, hivi karibuni aliteuliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuwa Mwakilishi Maalum kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, jukumu linalolenga kuimarisha juhudi za upatanishi, ushirikiano wa kikanda na utatuzi wa migogoro katika eneo hilo lenye changamoto za kiusalama na kisiasa.










No comments:
Post a Comment