SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUCHOCHEA MAENDELEO. - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, April 15, 2026

SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUCHOCHEA MAENDELEO.

Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Haule, akizungumza wakati akifungua warsha ya siku moja yenye lengo ya kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu na mashirika yasiyo ya kiserikali, iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Edema, mkoani Morogoro.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika mafunzo yaliyoratibiwa na Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, kwa lengo la kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu kuhusu ushirikiano wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania Bara, katika ukumbi wa hoteli ya Edema, mkoani Morogoro.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Omar Mkima, akiwasilisha mada kuhusu Mwongozo wa Uzingatiaji Fedha na Ushirikiano na Mashirika yasiyo ya Kiserikali, katika mafunzo yaliyoratibiwa na Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, kwa lengo la kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu kuhusu ushirikiano wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania Bara, katika ukumbi wa hoteli ya Edema, mkoani Morogoro.
Mchumi kutoka Wizara ya Fedha Bw. Elias Amede, akiwasilisha mada kuhusu Mwongozo wa bajeti ya Serikali, katika mafunzo yaliyoratibiwa na Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, kwa lengo la kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu kuhusu ushirikiano wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania Bara, katika ukumbi wa hoteli ya Edema, mkoani Morogoro.
Baadhi ya washiriki wakichangia hoja kuhusu mada zilizowasilishwa katika mafunzo yaliyoratibiwa na Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, kwa lengo la kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu kuhusu ushirikiano wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania Bara, katika ukumbi wa hoteli ya Edema, mkoani Morogoro.
Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Haule, akiwa katika picha ya pamoja washhiriki baada ya mafunzo yaliyoratibiwa na Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, kwa lengo la kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu kuhusu ushirikiano wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania Bara, katika ukumbi wa hoteli ya Edema, mkoani Morogoro.
----------------------------------------

Na. Saidina Msangi, WF, Morogoro.


Serikali imeweka bayana dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini, kwa lengo la kuhakikisha shughuli za mashirika hayo zinaendana na vipaumbele vya Taifa na kuchochea maendeleo jumuishi kwa wananchi.


Hayo yalibainishwa na Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Joseph Haule, wakati akifungua warsha ya siku moja yenye lengo ya kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu na mashirika yasiyo ya kiserikali, iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Edema, mkoani Morogoro.


Alisema warsha hiyo itawezesha washiriki kuelewa kuhusu ushirikiano kati ya Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali hapa nchini ili kuimarisha ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kijamii.


‘‘Jitihada za Serikali ya Tanzania zimekuwa zikilenga kuhakikisha kuwa maendeleo ya wananchi yanapatikana kwa njia jumuishi na endelevu. Katika kufikia azma hii, mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni muhimu sana, hasa katika kufikisha huduma kwa jamii na kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta mbalimbali’’, alisema Bw. Haule.


Alifafanua kuwa ili ushirikiano huo uwe na tija, kuna umuhimu wa kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mifumo, taratibu na miongozo inayosimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo.


‘‘Kuna umuhimu mkubwa kwa wadau kuelewa miongozo muhimu ikiwemo Mwongozo wa uzingatiaji fedha na ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali, Mwongozo wa Bajeti ya Serikali pamoja na Miongozo ya uratibu na ushirikiano wa maendeleo, hivyo kupitia warsha hii tunatarajia sote kujenga uelewa wa pamoja,’’ alisema Bw. Haule.

Aidha, warsha hiyo imetajwa kama jukwaa muhimu la kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Bw. Haule aliongeza kuwa ni matarajio ya Serikali kuwa kupitia majadiliano hayo, yatapatikana mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha mahusiano ya kikazi kati ya Serikali na wadau hao, pamoja na kuongeza uwazi, uwajibikaji na matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Kwa upande wao washiriki wa warsha hiyo wamebainisha kuwa kukutana kwa pande hizo mbili ni hatua ya kimkakati itakayosaidia kuunganisha huduma katika maeneo ambayo Serikali haijafika, huku mashirika hayo yakikamilisha juhudi za maendeleo kwa kufika maeneo ya ndani zaidi kutoa huduma kwa wananchi.


Aidha, walitoa rai kuwa mafunzo kama hayo yawe endelevu ili kuendelea kuwajengea uwezo wadau wote, hatua itakayohakikisha kuna kuwa na ushirikiano imara na endelevu katika kuleta mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi.


Mafunzo hayo ya siku moja yaliratibiwa na Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha kwa lengo la kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu kuhusu ushirikiano wa Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania Bara, kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Katavi pamoja na Morogoro.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad