𝐃𝐊𝐓. 𝐊𝐈𝐒𝐄𝐍𝐆𝐄 𝐀𝐖𝐀𝐏𝐎𝐍𝐆𝐄𝐙𝐀 𝐖𝐀𝐅𝐀𝐍𝐘𝐀𝐊𝐀𝐙𝐈 𝐉𝐊𝐂𝐈, 𝐀𝐒𝐈𝐒𝐈𝐓𝐈𝐙𝐀 𝐔𝐅𝐀𝐍𝐈𝐒𝐈 𝐍𝐀 𝐖𝐄𝐋𝐄𝐃𝐈 𝐊𝐀𝐙𝐈𝐍𝐈 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, May 1, 2026

𝐃𝐊𝐓. 𝐊𝐈𝐒𝐄𝐍𝐆𝐄 𝐀𝐖𝐀𝐏𝐎𝐍𝐆𝐄𝐙𝐀 𝐖𝐀𝐅𝐀𝐍𝐘𝐀𝐊𝐀𝐙𝐈 𝐉𝐊𝐂𝐈, 𝐀𝐒𝐈𝐒𝐈𝐓𝐈𝐙𝐀 𝐔𝐅𝐀𝐍𝐈𝐒𝐈 𝐍𝐀 𝐖𝐄𝐋𝐄𝐃𝐈 𝐊𝐀𝐙𝐈𝐍𝐈

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni moja na nusu Mfanyakazi Hodari wa taasisi hiyo nafasi ya tatu kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 Afisa Muuguzi Edna Kajuna wakati wa hafla ya kuwatambua na kuwapongeza wafanyakazi hodari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni mbili Mfanyakazi Hodari wa taasisi hiyo nafasi ya pili kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 Mkaguzi wa Hesabu za Ndani Sitty Hamis wakati wa hafla ya kuwatambua  na kuwapongeza wafanyakazi Hodari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa taasisi hiyo pamoja na wafanyakazi Hodari wa mwaka wa fedha wa 2025/2026 mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kuwatambua na kuwapongeza wafanyakazi Hodari iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa JKCI.

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

1/5/2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, amewapongeza wafanyakazi wa taasisi hiyo kwa kujituma na kufanya kazi kwa weledi hususan katika kuwahudumia wagonjwa wenye uhitaji maalum wakiwemo wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.


Dkt. Kisenge aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa mkutano wa wafanyakazi wa taasisi hiyo wa kuwatambua wafanyakazi hodari wa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo alisisitiza kuwa mafanikio ya taasisi hiyo yanatokana na mchango wa kila mfanyakazi.


Alieleza kuwa licha ya kutolewa kwa tuzo kwa baadhi ya wafanyakazi ukweli ni kwamba wafanyakazi wote ni hodari kutokana na mchango wao katika kuendeleza huduma za moyo nchini.


“Utaratibu wa kuchagua wafanyakazi bora ulifanyika kwa njia ya mfumo shirikishi wa kidijitali wa Best Employee System unaowezesha wafanyakazi kupiga kura kwa uwazi na haki”, alisema Dkt. Kisenge.


Aidha Dkt. Kisenge aliwataka viongozi wa taasisi hiyo kuwa karibu zaidi na wafanyakazi wanaowaongoza kwa kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati ili kuongeza ufanisi na ari ya kazi.


Pia alisisitiza umuhimu wa uwazi katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya kila idara pamoja na kuongeza wigo wa utoaji huduma ikiwemo kufanya upasuaji hata wakati wa sikukuu na mwishoni mwa wiki.


Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa JKCI, Ghati Chacha alisema ushindani wa kumpata mfanyakazi hodari ulikuwa mkubwa akibainisha kuwa kwa mara ya kwanza mchakato huo pia umehusisha ngazi za menejimenti na wasimamizi wa vitengo ili kuimarisha uwajibikaji katika kada zote.


Aliongeza kuwa utaratibu wa kuchagua wafanyakazi bora unafanyika kila mwaka kupitia mfumo wa kidijitali wa Best Employee System ambapo kila kurugenzi huchagua wawakilishi wake kabla ya kushindanishwa katika ngazi ya taasisi.


Kwa upande wake Mfanyakazi Hodari wa mwaka wa fedha 2025/2026 Afisa Utawala Adila Musa aliwashukuru wafanyakazi wenzake kwa imani waliyoonyesha kwake huku akisema ushindi huo ni wa pamoja kwani kila mfanyakazi ana mchango katika mafanikio ya taasisi.


Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa taasisi hiyo Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Moyo kwa Watoto Dkt. Sulende Kubhoja aliwahimiza wafanyakazi Hodari waliochaguliwa kuwa mfano bora kwa wenzao kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi huku akisisitiza kwa wafanyakazi wengine ambao hawakuchaguliwa umuhimu wa kuthamini na kusherehekea mafanikio ya wenzao.


Wafanyakazi hodari wa mwaka huu waliochaguliwa katika taasisi hiyo wote ni wanawake jambo linaloonesha kwa mchango mkubwa wa wanawake katika kuendesha na kuimarisha huduma za afya pamoja na kufanikisha malengo ya taasisi.


Afisa Utawala Adila Musa alishika nafasi ya kwanza kama Mfanyakazi Hodari wa mwaka wa fedha 2025/2026 akifuatiwa na Mkaguzi wa Hesabu za Ndani Sitty Hamis aliyeshika nafasi ya pili na Afisa Muuguzi Edna Kajuna aliyeshika nafasi ya tatu hatua inayoonesha wazi ufanisi na umahiri wa wanawake katika nyadhifa mbalimbali za kitaaluma ndani ya taasisi hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad