Meneja wa Masoko wa Kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA) wa Shelys Pharmaceutical – An Aspen Group Company, Bw. Ezekiel Muganda (kulia), akipokea kwa fahari Tuzo ya 21 ya Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) 2026 baada ya kampuni hiyo kuibuka mshindi (1st Runner-Up) katika kundi la Watengenezaji wa Bidhaa za Msingi za Dawa na Maandalizi ya Dawa.
...........................
Na Godwin Myovela, Njombe
Kampuni ya Shelys Pharmaceutical – An Aspen Group Company imeendelea kung’ara katika sekta ya afya na utengenezaji wa dawa baada ya kuibuka mshindi katika kundi la Watengenezaji wa Bidhaa za Msingi za Dawa na Maandalizi ya Dawa kwenye Tuzo za 21 za OSHA 2026.
Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika mkoani Njombe Aprili 29, 2026, yakihusisha viongozi wa serikali, waajiri na wadau mbalimbali wa kazi na ajira.
Shelys ilitunukiwa tuzo hiyo kutokana na kuendelea kuzingatia viwango vya usalama na afya mahali pa kazi pamoja na matumizi ya mifumo salama ya uzalishaji ndani ya kampuni.
Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa “Mazingira Bora ya Kisaikolojia Mahali pa Kazi: Njia ya Wafanyakazi wenye Mafanikio na Taasisi Imara,” ikisisitiza umuhimu wa ustawi wa wafanyakazi katika kuongeza tija na maendeleo ya taasisi.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa Masoko wa SSA wa kampuni hiyo, Bw. Ezekiel Muganda, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya mshikamano, taaluma na kujituma kwa wafanyakazi pamoja na menejimenti ya kampuni.
“Tunajivunia kupokea tuzo hii muhimu kutoka OSHA. Inaonesha dhamira yetu ya kuendelea kuwekeza katika afya, usalama wa wafanyakazi na ubora wa uzalishaji wa dawa,” alisema Bw. Muganda.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na juhudi za kila mfanyakazi wa Shelys anayehakikisha viwango vya kimataifa vinaendelea kuzingatiwa kila siku katika mazingira ya kazi.
Bw. Muganda pia aliishukuru OSHA kwa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha taasisi mbalimbali nchini kuweka mbele ustawi wa wafanyakazi na mazingira salama ya kazi kwa maendeleo ya taifa
Tuzo ikikabidhiwa.










No comments:
Post a Comment