𝗨𝗦𝗢𝗡𝗝𝗜 𝗪𝗔𝗠𝗧𝗘𝗦𝗔 𝗠𝗧𝗢𝗧𝗢 𝗦𝗪𝗔𝗨𝗠 𝗞𝗪𝗔 𝗠𝗜𝗔𝗞𝗔 𝟭𝟰 𝗬𝗨𝗣𝗢 𝗞𝗜𝗧𝗔𝗡𝗗𝗔𝗡𝗜, 𝗠𝗔𝗠𝗔 𝗬𝗔𝗞𝗘 𝗔𝗢𝗠𝗕𝗔 𝗠𝗦𝗔𝗔𝗗𝗔 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, May 3, 2026

𝗨𝗦𝗢𝗡𝗝𝗜 𝗪𝗔𝗠𝗧𝗘𝗦𝗔 𝗠𝗧𝗢𝗧𝗢 𝗦𝗪𝗔𝗨𝗠 𝗞𝗪𝗔 𝗠𝗜𝗔𝗞𝗔 𝟭𝟰 𝗬𝗨𝗣𝗢 𝗞𝗜𝗧𝗔𝗡𝗗𝗔𝗡𝗜, 𝗠𝗔𝗠𝗔 𝗬𝗔𝗞𝗘 𝗔𝗢𝗠𝗕𝗔 𝗠𝗦𝗔𝗔𝗗𝗔

Mtoto Swaum Shabani Machela (14) akiwa amepakatwa na Mama yake Sauda Selemani nyumbani kwao Pugu kwa Mustafa, Ilala Jijini Dar es Salaam.

.............................

MTOTO Swaum Shabani Machela (14) Mkazi wa Mtaa wa Kibong’wa Pugu kwa Mustafa Ilala Jijini  Dar es Salaam hajawahi kufurahia maisha kutokana na maradhi ya usonji aliyonayo.

Swaum ambaye wakati wote huwa anatabasamu huku akitamani kusimama na kutembea aweze kwenda shuleni kama ilivyo kwa watoto wengine lakini imekuwa ni kinyume muda wote amekuwa akilala kutokana na mwili wake kuwa dhoofu kwa maradhi hayo yaliyosababishwa na ukosefu wa chakula bora.

Mama wa mtoto huyo Sauda Selemani (39) anasema Swaum alizaliwa Septemba 2, 2013 nyumbani kwao katika Hospitali ya Magoma iliyopo Korogwe Mkoa wa Tanga.

Anasema alizaliwa akiwa na afya njema na kurejea nyumbani kwake Manzese Jijini Dar es Salaam alikokuwa akiishi na mume wake.

Sauda anasema mwanaye alipofikisha miaka minne hali yake ilianza kubadilika kila ilipofika usiku mwili wake ulikuwa ukipata joto kali na ndipo alipo mpeleka Hosptali ya Mwananyamala.

Anasema daktari aliyekuwa akimtibu alimuambia kuwa mwanaye alikuwa akisumbuliwa na nimonia ambapo alilazwa kwenye chumba cha joto kwa miezi minne lakini hali yake iliendelea kuteteleka.

Sauda anasema walilazimika kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambapo waligundua kuwa mwanaye alikuwa na utapiamlo ambao umemsababishia baadhi ya viungo vyake kudhoofu.

“Muhimbili nilikaa naye kwa wiki kadhaa akipatiwa chakula maalumu ambapo afya yake ilikuwa nzuri  kidogo ingawa mwili wake ulikuwa hauna nguvu ndipo nilipompeleka Hospitali ya CCRBT Msasani kwa ajili ya kufanyiwa mazoezi ya viungo.

Daktari alimuambia kutokana na lishe duni mtoto wake alikuwa amepatwa na usonji hivyo anatakiwa kumkazania awe anapata chakula cha kutosha na kufanya mazoezi hali yake itaimarika.

Sauda anasema anapita katika wakati mgumu mume wake naye ni mgonjwa wakati wote amekuwa na shinikizo la damu (presha) ambayo imekuwa ikimfanya awe anaanguka na kupoteza fahamu, hana kazi ya uhakika ya kumuingizia kipato.

Anasema yeye mwenyewe anachangamoto ya goti la mguu wa kulia kuvimba na kumsababishia kushindwa kutembea na maisha yao kwa ujumla hayaeleweki hata kula yao ni ya shida.

Mama huyo mwenye watoto watano anasema kama angeweza kupata mtaji angefanya chochote ili aweze kupata fedha za kuendesha maisha yao na kumtibu  mwanaye lakini amekwama kwa vile hawana kitu chochote cha kumuingizia kipato.

Aidha, Sauda amesema daktari amemuambia mwanaye akipata lishe bora, dawa za kutumia na kufanya mazoezi atapona, changamoto ni namna ya kupata fedha hizo.

“Swaum kutokana na hali yake mara nyingi amekuwa akizidiwa, juzi hali yake ilibadilika ghafla nikampeleka Muhimbili gharama ya dawa zake alizoandikiwa ilikuwa ni  zaidi ya shilingi 75,000 nimeshindwa kuzinunua zaidi ya panado alizopewa,” alisema Sauda.

Alisema changamoto nyingine aliyonayo ni namna ya kufika Hospitali ya Muhimbili akizidiwa mwanaye hasa nyakati za usiku kwani wanalazimika kutoka saa 9 usiku nyumbani kwao Pugu kwa Mustafa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa anaoishi Sauda Selemani, Shina namba 2, Emanuel Zakaria amethibitisha mama huyo kuwa na changamoto ya kimaisha.

“Serikali ya Mtaa anapoishi Sauda Selemani na familia yake tunaifahamu changamoto aliyonayo ni kweli anahitaji kusaidiwa,” alisema Zakaria kwa niaba ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwa Mustafa, Fikiri Selemani (Timbwa).

Ndugu Watanzania mmemsikia Sauda madhira anayopitia na familia yake anaomba msaada ili aweze kupata fedha au mtaji utakaomuwezesha afanye chochote ili apate fedha zitakazomsaidia kumtibu mwanaye na kuendesha maisha yao ya kila siku kwani kutoa ni moyo na wala siyo utajiri.

Kwa yeyote atakayeguswa kuishika mkono familia hiyo kwa chochote utakachojaaliwa na Mwenyezi Mungu hata kama utaona ni mdogo ziwe fedha, ushauri, chakula, Sabuni, chumvi, sukari na mahitaji mengine ya kibinadamu kwake utakuwa ni msaada mkubwa.

Unaweza kuwasiliana na mama huyo anayepita katika kipindi kigumu moja kwa moja kupitia  namba ya simu  0623757336 au 0625414791 jina litakalotokea ni Sauda Selemani Magwelo, Mungu atakubariki kwa utoaji wako.

Mtoto Swaum Shabani, akionesha tabasamu la matumaini, anakuomba msaada wako wewe unayemuangalia, uwe baba, mama, dada, kaka, mtoto mwenzake, kiongozi wa dini, mwanasiasa, mfanyabiashara, mwanafunzi na jamii kwa ujumla. Usimuache mtoto huyu bila ya kufanya chochote juu yake hata Sh. 2000 kwake itampa faraja na matumaini. Wasiliana na mama yake kwa namba ya simu hapo juu utabarikiwa mara 1000 kwa utoaji wako.

Mama mzazi wa Swaum, Sauda Selemani, akiwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa anaoishi Shina namba 2, Pugu kwa Mustafa Jijini Dar es Salaam, Emanuel Zakaria.

........................

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad