BIBI KIZEE AMLILIA RAIS SAMIA AMSAIDIE BAADA VIONGOZI WA KIJIJI KOROGWE, KUFYEKA MAZAO KATIKA SHAMBA LAKE - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 20 December 2023

BIBI KIZEE AMLILIA RAIS SAMIA AMSAIDIE BAADA VIONGOZI WA KIJIJI KOROGWE, KUFYEKA MAZAO KATIKA SHAMBA LAKE

Bibi Zaina Waziri Kipanga (88) Mkazi wa Kijiji cha Kwakombo Kata ya Kwakombo wilayani Korogwe mkoani Tanga, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akimuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati mgogoro wa ardhi dhidi yake na Serikali ya Kijiji cha Kwamsisi. 

...............................................

Na Dotto Mwaibale, Korogwe

BIBI kizee Zaina Waziri Kipanga (88) Mkazi wa Kijiji cha Kwakombo Kata ya Kwakombo wilayani Korogwe mkoani Tanga amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati apate haki yake kufuatia Serikali ya Kijiji cha Kwamsisi kufyeka mazao ya mahindi katika shamba lake kutokana na mgogoro wa ardhi dhidi yake na Serikali ya kijiji hicho.

Kikongwe huyo amedai kwamba licha ya viongozi wa Wilaya ya Korogwe kuufahamu mgogoro huo wameshindwa kumsaidia hali inayoonesha kuwa kuna njama za makusudi za kutaka kumdhurumu shamba shamba lake.

Akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni Bibi Kipanga alisema amelazimika kumuomba Rais amsaidie kwa kuwa hajui  hatima ya maisha yake kwani hana chakula wala shamba baada ya Serikali ya Kijiji cha Kwamsisi kumnyang'anya shamba lake la ekari 12 alilokuwa akilitumia na mume wake Waziri Kipanga ambaye sasa ni marehemu wakidai ni mali ya kijiji hicho.

Alisema kutokana na mgogoro huo mahindi aliyolima msimu huu wa kilimo yamefyekwa na Serikali ya kijiji hicho na kutakiwa wasiingie kwenye shamba hilo ambalo wamekuwa wakilima tangu wakati wa oparesheni vijiji iliyofanyika miaka ya 70.

Aliongeza kuwa viongozi hao wamekusudia kuwanyang'anya shamba lake hilo kwa hila kwani katika shamba hilo kuna mazao yao ya kudumu kama miembe, minazi, miti aina ya mitiki na makaburi ya familia hiyo.

Bibi Kipanga alisema kuwa kabla ya marehemu mume wake hajafariki wakiwa nyumbani kwao na mke mwenzake walifika watu na kuwaambia kuwa wamepita kwenye eneo la shamba hilo ambapo wamekuta kuna magari na watu wanajenga nyumba kwenye shamba lao.

Alisema baada ya kuambiwa hivyo walikwenda katika eneo hilo na kukukuta ni kweli kuna ujenzi ukiendelea na walipohoji waliambiwa kuwa kuna mradi wa ufugaji wa ng' ombe wa maziwa unatarajiwa kuanzishwa kwenye hilo lakini hawakuambiwa ni nani aliyetoa eneo kupisha mradi huo.

Alisema mradi huo haukuwahi kufanya kazi tangu wakati huo mpaka ikafikia hatua ya majengo hayo yaliyojengwa kubomoka lakini wao na mume wao walikuwa wakiendelea kulima katika shamba hilo hadi hivi sasa ambapo Serikali ya kijiji hicho ilipoibuka na kudai ni la kwao na kufikia hatua ya kufyeka mazao yao huku wakikata minazi na mazao mengine ya kudumu jambo ambalo linawashangaza.

Aliongeza kuwa suala hilo lilifikishwa hadi kwenye vyombo mbalimbali vya sheria lakini Serikali ya kijiji hicho imeshindwa kuthibitisha uhalali wa kudai shamba hilo ni lao.

Alisema ekari hizo 12 zipo ndani ya ekari nyingine 38 ambazo mradi huo ulikuwa ufanyike lakini ekari hizo ziliuzwa na watu waliokuwa wakilima lakini cha kushangaza waliouza wapo na wala hawajachukuwa hatua yoyote jambo ambalo linaonesha kuna hila inafanyika dhidi yao.

Watoto wa bibi huyo, Said Waziri Kipanga, Mariam Waziri Kipanga, Mkiwa Waziri Kipanga na Abdallah Waziri Kipanga ambao sasa ni watu wazima wanasema tangu opareshini ya vijiji wakiwa watoto wazazi wao walikuwa wakiishi katika eneo hilo na wanashngaa kuona Serikali ya kijiji hicho ikiwafukuza katika shamba lao hilo.

"Tangu tukiwa watoto wazazi wetu walikuwa wakilima katika shamba letu hilo namaliza shule naolewa na watoto wangu wanakuwa wanajua hilo shamba ni la babu yao Mzee Kipanga inatushangaza kuona tukiambiwa tuondoke tuende wapi tunakuomba Rais Samia Mama yetu wa huruma utusaidie tupate haki yetu," alisema Mariam Kipanga.

Said Kipanga ambaye ndie aliyechaguliwa kusimamamia mirathi baada ya baba yao kufariki amesema amepata misukosuko mingi ikiwemo ya kuwekwa mahabusu mara kwa mara kwa ajili ya kufuatilia jambo hilo.

Anasema licha ya kuweka tangazo la mirathi kwa muda wa miezi mitatu  kuhusu mali za baba yao likiwemo shamba hilo hakuna mtu yeyote ambaye alijitokeza kupinga lakini wanashangaa Serikali ya kijiji hicho kuanza kujitokeza hivi sasa wakidai shamba hilo ni mali ya Serikali.

Mkazi wa kiji hicho Hemedi Mwigole ambaye alikuwa na shamba lake kwenye eneo hilo linalodaiwa kuwa ni la mradi anasema familia hiyo haitendewi haki kwani mashamba hayo yalikuwa ni ya wazazi wao tangu wakati wa opareshini vijiji na kuwa baba yake ndiye aliyemkaribisha mzee Kipanga katika eneo hilo.

"Hapa kuna ujanja ujanja tu unafanyika mimi shamba langu nililiuza sasa kama liklikuwa ni la Serikali mbona sijawahi kuulizwa na mtu yeyote na Seriklali ya kijiji chetu ilikuwepo" alihoji Mwigole huku akitaka wafuatiliaji wa jambo hilo waingie kiundani kupata historia ya mashamba hayo.

Mwenyekiti Mstaafu wa Kijiji hicho, Hamadi Mwinyimsanga tangu aliyeshika madaraka tangu mwaka 1983 hadi mwaka 2006 anasema kwa kipindi chote hicho cha nyuma hakukuwepo na chokochoko hizo za kudai shamba la familia ya Kipanga ni mali ya kijiji na wala hakuwahi kuona vielelezo vyovyote vinavyoonesha uhalali huo.

"Sisi wakati wa uongozi wetu kwa kuzingatia shamba hilo lilikuwa likitumiwa na familia hiyo tangu wakati wa oparesheni vijiji na baada ya kuona hakuna mradi unaoendelea katika eneo hilo licha ya kujengwa miundombinu kama josho na mabanda tuliridhia familia hiyo kuendelea kulima shamba hilo ambalo lilikuwa na ekari zaidi ya 15 hivi," alisema Mwinyimsanga.

Alisema mradi huo haukufanikiwa kutokana na kutokidhi kwa vigezo na hata kwenye ramani ya kijiji hicho hakuna sehemu inayoonesha kuwepo kwa mradi na baada ya hapo kila mtu aliyekuwa na shamba lake kwenye eneo hilo aliendelea kulima huku wengine wakiyauza.

Mwinyimsanga anasema tangu mwaka 1972 hadi alipokuwa akistaafu nafasi yake ya Mwenyekiti mwaka 2006 hakukuwepo na changamoto yoyote kuhusu shamba hilo na hata viongozi wengine waliofuatia waliendelea kuiachia familia hiyo kuendelea kulitumia shamba hilo la marehemu baba yao.

Alisema mamlaka mbalimbali zimejaribu kulifuatilia  jambo hilo lakini bado haioneshi kama haki inatendeka kwa familia hiyo ambapo baadhi ya viongozi wa kijiji hicho wakituhumiwa kuhusishwa na njama za kunyang'anya shamba hilo kwa ajili ya kujijenga kisiasa  wakitaka kutumia eneo hilo kwa ajili ya kuanzisha mnada.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Salehe Msisi akizungumzia suala hilo alisema wakati anaingia madarakani alikabidhiwa eneo hilo na viongozi waliomtangulia likiwa na miundombinu ya josho na baadhi ya mabanda na alielezwa kuwa ni mali ya Serikali hata hivyo hakuweza kueleza kama kijiji hicho kina hati ya umiliki wa eneo hilo.

Msisi alipotakiwa kuzungumzia ufyekaji ya mazao yaliyo pandwa na familia hiyo alisema wamekuwa wakilifanyia usafi eneo hilo lakini hajawahi kupata taarifa yoyote ya mazao kufyekwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Tito Mganwa akizungumzia kuhusu mgogoro huo alikiri kuufahamu  na kueleza kuwa eneo hilo ni mali ya halmashauri hiyo na awali lilikuwa likimilikiwa na Serikali ya kijiji cha Kwamsisi na lilikuwa na miundombinu ya mifugo kama josho na nyumba ya mtumishi.

Alisema katika eneo hilo kuna ekari kama 50 ambazo halmashauri hiyo imetenga kwa ajili ya kuanzisha mnada kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa wananchi wa kijiji hicho cha Kwamsisi na kuwa wamekwisha tenga fedha na mwaka huu wa fedha wa 2023/ 2024 wanatarajia kujenga miundombinu kwa ajili ya kuanza rasmi mnada huo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Tito Mganwa akizungumzia kuhusu mgogoro huo. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwamsisi, Salehe Msisi akizungumzia suala hilo.
Bibi Zaina Waziri Kipanga (88) akiwa na watoto wake Mariam na Mkiwa Kipanga.
Mtoto wa Bibi Zaina Kipanga, Said Kipanga akiwa na huzuni wakati akizungumzia tukio hilo kwa waandishi wa habari.
Mkazi wa kijiji hicho, Hemed Mwigole, ambaye alikuwa akimiliki shamba katika eneo hilo la mgogoro akizungumza.
Mtoto mkubwa wa Bibi Zaina, Abdallah Kipanga akizungumzia mgogoro huo.
Mtoto wa bibi huyo, Mariam Kipanga, akizungumza.
Mtoto wa Bibi Zaina, Mkiwa Kipanga, akizungumza.
Mwenyekiti Mstaafu wa Kijiji hicho, Hamadi Mwinyimsanga, akizungumzia tukio hilo.
Baadhi ya mazao yaliyopandwa na familia ya Kipanga katika shamba hilo.
Baadhi ya wanafamilia ya Waziri Kipanga wakiwa kwenye shamba hilo walipokuwa na waandishi wa habari waliofika kuliona.
Baadhi ya wanafamilia ya Marehemu Mzee Waziri Kipanga na wananchi wakiangalia josho ambalo lilitelekezwa baada ya kuanzishwa kwa mradi huo wa ng'ombe.
Baadhi ya familia ya Mzee Kipanga na baadhi ya wananchi wakiwa wameshika mabaki ya ukuta ya lililokuwa banda la ng'ombe la mradi huo ambao haukufanyika.
Baadhi ya ndugu wa marehemu mzee Waziri Kipanga wakiwa mbele ya baadhi ya makaburi ya ndugu zao yaliyopo kwenye shamba hilo.
Baadhi ya miembe iliyopo kwenye shamba hilo.
Watoto wa Marehemu Mzee Waziri Kipanga, Maria na Mkiwa wakiokota mabua ya mahindi yanayodaiwa kubakia baada ya viongozi wa kikiji cha Kwamsisi kudaiwa kuyafyeka.
....................................

 ANGALIA VIDEO CHINI

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad