POLISI SINGIDA, LATRA WAFANYA OPERESHENI KUBAINI MADEREVA WANAOENDESHA MAGARI WAMELEWA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 20 December 2023

POLISI SINGIDA, LATRA WAFANYA OPERESHENI KUBAINI MADEREVA WANAOENDESHA MAGARI WAMELEWA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutahibirwa (kulia)  Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa Mrakibu wa Polisi (SP) Nestory Didi (kushoto) na Mkaguzi wa Polisi, Miguta Kubilu  na mmoja wa dereva wa mabasi makubwa wakiangalia kipimo cha kupima kubaini kama dereva amekunywa kilevi wakati wa operesheni ya ukaguzi wa magari na utoaji wa elimu kwa abiria iliyofanyika Disemba 19, 2023 Stendi Kuu ya Mabasi ya Misuna.

.......................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida 

JESHI la Polisi Mkoa wa Singida kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) linaendelea na operesheni maalum ya kukagua mabasi na madereva kama wamekunywa pombe ili kudhibiti ajali ambazo zimekuwa zikijitokeza kipindi cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Pia, LATRA na jeshi hilo wanaendelea kutoa elimu kwa madereva,makondakta wa mabasi na kwa abiria ili wanapoona dereva anaendesha mwendo kasi ambao unahatarisha usalama wao waweze kutoa taarifa .

Akizungumza wakati akiongoza operesheni hiyo iliyofanyika Kituo Kikuu cha Mabasi  Misuna,  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Stella Mutahibirwa  alisema operesheni hiyo wanayoifanya inalenga kuhakikisha magari yote yanayoingia Mkoa wa Singida yanaingia na kutoka yakiwa salama.

Alisema katika operesheni hiyo wamebaini kuwa mabasi mengi hayana mikanda ya usalama na iliyopo ni mibovu na akaongeza kuwa changamoto nyingine ni wazazi wanaposafiri na watoto wao zaidi ya wawili kutowakatia tiketi za siti zao jambo ambalo sio nzuri kiusalama .

Alisema madereva wanapoingia katika kituo hicho cha mabasi huwapima kama wamekunywa pombe kwa kutumia kifaa maalumu na kutoa elimu kwa abiria kuwa wanaposafiri na kuona dereva anakwenda mwendo wa kasi watoe taarifa kwa jeshi la polisi kupitia namba za wakuu wa jeshi hilo zilizopo kwenye mabasi hayo.

” Sisi Jeshi la Polisi jukumu letu ni kulinda maisha ya raia na mali zao hivyo tumeamua kufanya operesheni hii ya kutoa elimu kwa abiria ili waweze kujua haki zao na kutoa taarifa pale wanapoona madereva wakiendesha mwendo kasi," alisema Mutahibirwa.

Alisema wamezungumza na abiria na madereva kuhusu wajibu wao wanapokuwa wanaendesha magari na kuwataka kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa za usalama barabarani na kuhakikisha wanawafikisha abiria wao salama wanakokwenda na kuwa kauli mbiu yao ya mwaka huu inasema ‘ukimya wako ni umauti wako paza sauti.

Aidha, Mutahibirwa  alisema abiria nao wanajukumu la kuwasaidia jeshi la polisi kukemea  maovu yanayofanyika pindi wanapokuwa kwenye safari yakiwemo ya mwendo kasi na dereva anayeyapita magari mengine kwa wakati mmoja na eneo ambalo sio sahihi.

Aliwataka abiria wakati wote wanaposafiri kujenga tabia ya kufunga mikanda ambayo imewekwa mahususi kuwasaidia pale gari husika litakapopata changamoto ya dereva wake kusisima kwa ghafla au kupata ajali.

"Jambo la kwanza unapopanda ndani ya gari ni kuhakikisha unafunga mkanda kwenye siti yako na kama haina mkanda ni vema ukatoa taarifa kwa kondakta," alisema Mutahibirwa.

Mutahibirwa aliwaambia abiria hao wawe wasaidizi wa jeshi la polisi kwa kutoa taarifa kuhusu uendeshaji usiofaa wa dereva husika na kuwa maisha yao yanathamani sana kwao na kwa taifa hivyo aliwaomba wapaze sauti wanapoona mambo hayo ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yao.

Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mkoa wa Singida, Layla Dafa akizungumza kwenye operesheni hiyo alisema wamekuwa wakiyakagua mabasi hayo ili kubaini makosa mbalimbali ambayo yanafanywa na madereva na makondakta moja ya makossa hayo ni kutowakatia abiria tiketi za kielektoniki ambapo wamewasisitizia sana abiria kutumia tiketi hizo ili wasizidishiwe nauli wanaposafiri.

Aidha, alisema wamewaelekeza makondakta na madereva wanapoweka mizigo ya abiria chini ya buti wawe wanaweka alama za kuonesha majina ya wenye mizigo hiyo wanaosafiri nao ili kuepusha kuchukuliwa na abiria wengine na kuwa mizigo inakuwa chini ya dhamana yao hivyo wanapaswa kuitunza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Mawaka wa Mabasi Stendi Kuu ya Misuna, Msafiri Ndui alisema wakati wote unapofika msimu wa abiria wengi baadhi ya mawakala wasiowaaminifu wamekuwa wakipandisha bei ya nauli lakini wao wamekuwa wakidhibiti hali hiyo kutokana na utaratibu waliojiwekea.

“Tunautaratibu wetu tuliojiwekea hairuhusiwi kupandisha nauli na ni lazima abiria aandikiwe bei elekezi na akitokea wakala kukiuka kuna adhabu zetu ambazo tumeziweka,” alisema Ndui.

Mkaguzi wa Polisi, Miguta Kubilu, akimpima mmoja wa madereva wa mabasi makubwa kwa ajili ya kubaini kama atakuwa ametumia kilevi cha aina yoyote wakati wa operesheni hiyo ya ukaguzi wa magari na utoaji wa elimu kwa abiria iliyofanyika Disemba 19, 2023 Stendi Kuu ya Mabasi ya Misuna.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutahibirwa, akitoa elimu kwa abiria wakati wa operesheni hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutahibirwa, akiongoza maafisa wa polisi wakati wa operesheni hiyo.
Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mkoa wa Singida, Layla Dafa akizungumza kuhusu operesheni hiyo. 
Mwenyekiti wa Umoja wa Mawaka wa Mabasi Stendi Kuu ya Misuna, Msafiri Ndui, akizungumzia operesheni hiyo. 
Maafisa wa polisi wakiwa kwenye opereshini hiyo.
Askari wa usalama barabarani wakiwa kwenye operesheni hiyo.
Taswira ya operesheni hiyo katika stendi hiyo ya mabasi ya Misuna.
..................................

ANGALIA  VIDEO CHINI

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad