BIBI KIZEE, RC TANGA WANYUKANA MGOGORO WA ARDHI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, 26 December 2023

BIBI KIZEE, RC TANGA WANYUKANA MGOGORO WA ARDHI


 Bibi kizee Zaina Waziri Kipanga (88) Mkazi wa Kijiji cha Kwakombo Kata ya Kwakombo wilayani Korogwe mkoani Tanga, ambaye anamuomba Rais Samia Suluhu Hassan amesaidia kuingilia kati mgogoro wa ardhi dhidi ya Serikali ya Kijiji cha Kwamsisi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba


..................................................


Na Dotto Mwaibale, Korogwe

SAKATA la Bibi kizee Zaina Waziri Kipanga (88) Mkazi wa Kijiji cha Kwakombo Kata ya Kwakombo wilayani Korogwe mkoani Tanga aliyemuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati apate haki yake kufuatia Serikali ya Kijiji cha Kwamsisi kudaiwa kufyeka mahindi katika shamba lake kutokana na mgogoro wa ardhi dhidi yake na Serikali ya kijiji hicho limechukua sura mpya.

Mgogoro huo umechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba kuibuka na kutoa ufafanuzi ambao unapingwa vikali na familia ya Kipanga wakidai anadanganywa na viongozi wa Wilaya ya Korogwe.

Mwandishi wa habari hii aliyepata fursa ya kutembelea eneo hilo linalodaiwa kuwa na mgogoro ameshuhudia makaburi, miembe, sambamba na magofu ya vibanda vya miundombinu ya mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Hata hivyo kwa kuzingatia heshima, ustawi na utu wa Mtanzania Serikali inapaswa kuutazama mgogoro huo kwa jicho la pili kwa kuipa shamba lingine familia hiyo ili kuinusuru kwa kuwa haina sehemu yoyote ya kimaendeleo ambayo itawasaidia kujipatia mahitaji ya msingi ya maisha.

Akizungumza hivi karibuni na vyombo vya habari, Bibi Kizee  huyo alidai kwamba licha ya viongozi wa Wilaya ya Korogwe kuufahamu mgogoro huo wameshindwa kumsaidia hali inayoonesha kuwa kuna njama za makusudi za kutaka kumdhurumu shamba lao na mke mwenzie lenye ekari 12 ambalo liliachwa na mume wao Waziri Kipanga aliyefariki Oktoba 9, 1998 walilokuwa wakilitumia kwa kilimo tangu wakati wa oparesheni vijiji ya miaka ya 70.

Akitoa ufafanuzi huo baada ya kupewa maelezo na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kindamba alisema familia ya Omary Kipanga imekuwa ikilalamika juu ya Ardhi ya Kwamsisi kwa muda mrefu na kuwa hakuna mahindi wala mazao yao yaliyoharibiwa na Kijiji cha Kwamsisi  au Halmashauri ya Korogwe TC kwa mwaka 2023. 

RC Kindamba akizungumzia historia fupi ya jambo hilo alisema mwaka 2021 mlalamikaji alipeleka malalamiko Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tanga, 

Alisema utatuzi ulifanyika kwa kufuata taratibu zote na  hitimisho lilitolewa ni kuwa eneo hilo lenye mgogoro ni mali ya Serikali ya Kijiji cha Kwamsisi ambapo familia hiyo ilishauriwa kuomba eneo kwenye Serikali ya kijiji kama ambavyo wengine huomba kwa ajili ya kilimo lakini  haikufanya.hivyo. 

Kindamba aliongeza kuwa mwaka huu 2023 familia hiyo iliingia eneo hilo la mgogoro na kung'oa miti 500 iliyokuwa imepandwa na idara ya mifugo ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mji iliwafungulia kesi Mahakama ya Old Korogwe kesi Namba 59/2023 na kueleza kuwa  inasimamiwa na wakili wa Serikali ambaye aliomba  iendeshwe ngazi ya wilaya na kuwa utaratibu unaendelea. 

Alisema eneo hilo la mgogoro kwa muda mrefu Halmashauri hiyo ilipanga kuanzisha mnada wa mifugo na katika mwaka huu wa fedha kati ya Agosti na Septemba kijiji hicho kimekuwa na harambee ya kusafisha eneo hilo. 

“ Katika eneo hilo upo ushahidi tosha kwamba toka mwaka 1978 Serikali iliweka miundombinu kadhaa kama Josho na vyoo hivyo kupitia taarifa hii naomba kuwasilisha kuwa eneo hili ni mali halali ya Halmashauri  kupitia Kijiji cha Kwamsisi,” alisema Kindamba. 

Msimamizi wa mirathi ya shamba hilo ambaye ni mmoja wa watoto wa Omari Kipanga alisema tangu opareshini ya vijiji iliyofanyika miaka ya 1970 wazazi wao walikuwa wakiishi katika eneo hilo na wanashngaa kuona Serikali ya kijiji hicho ikiwafukuza kwa madai shamba hilo ni lao.

Alisema baada ya baba yao kufariki mwaka 1998 na kuwaacha watoto 10 na mali kadhaa na mashamba manne likiwepo  hilo lenye mgogoro Februari 1, 2019 walifungua shauri la mirathi Namba 01/2019 Mahamama ya Mwanzo ya Hakimu Mkazi Manundu Korogwe muombaji akiwa Said Waziri  Kipanga aliyechaguliwa na familia na kuthibitishwa na mahakama hiyo Julai 31, 2019.

Alisema baada ya kuthibitishwa lilitolewa tangazo la mirathi  ambalo lilibandikwa kwenye mbao za matangazo za ofisi ya kijiji cha Kwamsisi kwa muda wa miezi mitatu lakini hakukuwepo mtu yeyote aliyejitokeza wala uongozi wa Serikali ya kijiji hicho kupinga uhalali wa familia hiyo kumiliki mali hizo pamoja na shamba hilo ambalo lipo umbali usio zidi mita 100 kutoka ilipo ofisi hiyo.

Said alikiri mazao yao kuharibiwa ikiwemo minazi na alikanusha familia hiyo kufyeka miche 500 iliyopandwa na halmashauri ambapo walifunguliwa kesi namba 59/2023.

Alisema kesi hiyo ilikuwa ni ya kutengenezwa kwa lengo la kudhohofisha kasi ya kufuatilia haki ya kupata shamba hilo na kuwa Julai 10, 2023 Mkurugenzi wa Mashitaka kupitia kwa mkuu wa mashitaka wa wilaya ya Korogwe alitoa hati ya kulifuta shauri hilo baada ya upande wa ulalamikaji kushindwa kuhudhuria mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi unaothibitisha familia hiyo kufanya kosa hilo.

Said Kipanga alisema familia hiyo inashangaa kuona Serikali ya Kijiji cha Kwamsisi inaposhindwa kuheshimu mamlaka ya mahakama ambayo ilitangaza kufungua mirathi ambapo wanaendelea kudai ardhi hiyo ni yao wakati ikijua fika ni mali ya familia ya Mzee Kipanga.

Kipanga alisema Serikali ya kijiji hicho hata siku moja haijawahi kuishauri familia hiyo kuomba shamba lingine kama alivyoeleza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba ambaye ameombwa kwenda kijijini hapo kupata historia halisi ya shamba hilo kwani waliojenga miundombinu ya mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa waliuanzisha bila ya kuishirikisha familia hiyo ambayo ilikuwa ikilima shamba hilo kwa muda mrefu.

Bibi kizee Zaina Waziri Kipanga (88) (kulia) akiwa na watoto Mariam Kipanga na Mkiwa Kipanga wakati wakizungumza na waandishi wa habari.
Msimamizi wa mirathi, Saidi Kipanga, akiwa na huzuni kufuatia tukio hilo.
Baadhi ya Wanafamilia hiyo na wananchi wakiwa mbele ya makaburi ya familia yaliyopo kwenye shamba hilo. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad