KANISA LA ABC LAWAKUMBUKA WAJANE, WAHITAJI- KRISMASI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 27 December 2023

KANISA LA ABC LAWAKUMBUKA WAJANE, WAHITAJI- KRISMASI


Askofu Kiongozi wa Kanisa  la Abundant Blessings (ABC) la Tabata Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila akizungumza wakati wa hafla ya kushiriki chakula cha pamoja na wajane, wagane na watu wenye uhitaji iliyoandaliwa na kanisa hilo jana.

Na Kulwa Mwaibale 

KANISA la Abundant Blessings (ABC) la Tabata Mandela jijini Dar es Salaam limewakumbuka wajane, wagane na wahitaji wengine katika kusherekea Sikukuu ya Krismasi kwa kula pamoja. 

Tukio hilo lililokwenda sambamba na kula chakula cha pamoja, lilijiri jana kanisani hapo ambapo walengwa hao walipewa maneno ya faraja na kuwatia moyo wajane na  Mchungaji Colleta Makula wa Kanisa la EAGT Mabibo, Dar aliyefiwa na mumewe Mwaka 1994. 

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Askofu Kiongozi wa Kanisa hilo, Flaston Ndabila alisema Mwaka huu wameamua kula chakula cha pamoja na kundi Hilo tofauti na miaka iliyopita ambapo waliwagawia chakula na vitu vingine. 

"Mwaka huu tumeamua kufanya tofauti, tumeamua tule, tunywe tufurahi pamoja," alisema Ndabila. 

Aliongeza kuwa baada ya chakula kila mmoja atapata bahasha itakayo kuwa na senti kidogo kwa ajili ya kwenda nayo nyumbani kwa ajili ya watoto na watu wengine ambao hawakuweza kuhudhuria haraka   hiyo. 

Mchungaji Makula aliyekuwa mgeni rasmi aliyeandaliwa kuwapa maneno ya faraja wajane, aliwaasa wasiwe watu wa kunung'unika bali wasimame na Mungu anayewapenda na kuwaangalia wajane kuliko watu wote duniani. 

"Wajane wenzangu msiwe watu wa kunung'unika kwa kufiwa na wenza wenu, simameni na Mungu atawatendea makubwa kama aliyonitendea mimi, " alisema mchungaji huyo ambaye mumewe alipofariki dunia na kumuachia watoto nane. 

Aliwaasa wasipende kuwafuata ndugu wa waume zao kuomba msaada hususan waliowatelekeza baada ya kufiwa wamtegee Mungu wa wajane na yatima. 

Mchungaji huyo aliwatia moyo wajane hao kwamba Kwa kumtegemea Mungu amefanikiwa kuwasomesha watoto wote ambao baadhi Yao wana kazi na tayari anawajukuu akiwepo anayesoma chuo. 

Alisema, wajane huheshimiwa sana kwenye jamii hivyo waishi Kwa kumtanguliza Mungu atakayewatendea Makuu. 

Mchungaji Oliver Ng'erumba wa Kanisa la EAGT Morogoro ambaye pia ni mjane aliwaasa wajane wenzake kutokata tamaa baada ya waume zao kutangulia kuondoka duniani badala yake wamuombe Mungu awapambanie Kwa kila jambo watashuhudia Makuu kama yanayotokea kwenye maisha yake ambayo ni ya furaha badala ya huzuni. 

Bi Asha Mziwanda ambaye ni mjane amemshukuru Ndabila Kwa moyo wa upendo kwao ambapo amesema anawajali wajane na wahitaji wengine.

"Kila Mwaka wakati huu wa Krismasi huyu Askofu wa Kanisa hili anashiriki nasi Kwa kutupatia chakula, vitu vingine na fedha, Mungu ambariki na Kanisa lake,' alisema Mziwanda. 

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mandela, Tabata, Tabrisa Abushir aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Serikali WA mtaa huo, alimshukuru Ndabila Kwa kuwajali wajane na wahitaji wengine. 

Amewaomba wakazi wa mtaa wa Mandela kushirikiananaye Kwa mambo mbalimbali zikiwemo  nyakati za huzuni na furaha. 

Mjumbe huyo ambaye pia ni kiongozi wa Jumuiya ya vijana ya CCM kwenye mtaa WA Mandela wanatarajia Desemba 31 siku ya mkesha WA Mwaka Mpya kumzawadia Askofu huyo ikiwa kumshukuru Kwa anavyojitoa Kwa jamii ya mtaa huo.

Askofu Ndabila akisisitiza jambo kwenye hafla hiyo.

 Askofu Kiongozi wa Kanisa hilo, Flaston Ndabila akitoa msaada huo kwa mmoja wa wagane .
Hafla hiyo ikiendelea.
Mchungaji Colleta Makula wa Kanisa la EAGT Mabibo, Dar akizungumza kwenye tukio hilo.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo na wahitaji wakishiriki hafla hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad