MBUNGE IRAMBA MASHARIKI AKABIDHI RADIO KWA WACHUJA NAFAKA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 27 December 2023

MBUNGE IRAMBA MASHARIKI AKABIDHI RADIO KWA WACHUJA NAFAKA

Mbunge wa  Iramba Mashariki, Mhe.Francis Isack Mtinga, akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Mbuyuni wakati alipokuwa kwenye hafla ya kukabidhi radio kwa wanawake Wachuja Nafaka katika tukio lililofanyika jana, Iguguno wilayani Mkamalama mkoani Singida. 

Na Dotto Mwaibale, Singida

MBUNGE  wa Jimbo la Iramba Mashariki, Mhe.Francis Isack Mtinga ametimiza ahadi yake kwa kutoa radio kwa Wajasiriamali Wanawake wanaojishughulisha na uuzaji wa pombe za asili (WACHUJA NAFAKA)  inayotengenezwa kwa kutumia nafaka wa Kitongoni cha Mbuyuni Kata ya Iguguno wilayani Mkalama mkoani Singida.

Akizungumza jana wakati akikabidhi radio hiyo Mtinga alisema wanawake hao walikuwa na changamoto ya kukodi radio kila siku walipokuwa wanafanya biashara yao ya kuuza pombe hiyo ya asili kwa ajili ya kuwaburudisha wateja wao na kusababisha kupata kipato kidogo.

Alisema wanawake hao walimuomba awasaidie kununua radio hiyo ili waondokane na changamoto ya kukodi radio kila wakati wanapokuwa kwenye biashara yao.

"Leo siku ya Boxing Day nimeona nifike kwa ajili ya kutekeleza ahadi yangu ya kuwapa radio itakayowasaidia kuwaburudisha wateja wenu hivyo kuongeza kipato chenu kwa kuzingatia kuwa ninyi ni jeshi kubwa na mnategemewa na watu wengi,” alisema Mtinga.

Baadhi ya wachuja nafaka hao walimshukuru mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi yake hiyo na kumuelezea kuwa ni mbunge anayejali wananchi wake wote kwa ujumla.

“Mbunge wetu  Mtinga ni mtu wa vitendo zaidi na kama mnavyoona katuleetea radio ambayo itakuwa ikitupa burudani wakati tunapata kinywaji chetu cha asili pamoja na kutuhabarisha mambo mbalimbali ya maendeleo,” alisema mmoja wa wanawake hao wachuja nafaka.


Wadau wakizungumza kwenye hafla hiyo wakati wakitoa shukurani kwa mbunge huyo.
Hafla hiyo ikiendelea. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad