Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Gwau akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chama na maendeleo alizozifanya katika kipindi cha mwaka 2022/ 2023 katika kikao maalumu cha Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kilichofanyika Disemba 23, 2023.
..................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Gwau ametoa taarifa ya
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chama na maendeleo alizozifanya katika
kipindi cha mwaka 2022/ 2023.
Akitoa taarifa hiyo katika kikao maalumu cha Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) Mkoa wa Singida kilichoketi Disemba, 23, 2023 alianza kwa kutoa pongezi
kwa Wanawake wa Mkoa wa Singida kwa kujitoa kwa wingi na mapokezi mazuri walioyafanya kwa viongozi mbalimbali wa
kitaifa waliofika kwa ziara za kikazi mkoani
hapa kwa nyakati tofauti na kuufanya mkoa wa Singida kung'ara ukilinganisha na
mikoa mingine.
Alitaja ziara za viongozi hao kuwa ni ile aliyoifanya Rais Samia Suluhu
Hassan, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo na Mwenyekiti wa
UWT Taifa, Mary Chatanda.
Gwau akielezea baadhi ya mambo aliyochangia ni michango ya vikao vya chama
kuanzia ngazi ya wilaya na mkoa kwa kutoa fedha kwa ajili ya kununulia chakula.
maji na mahitaji mengine ikiwemo mchango wa uchaguzi wa chama kuanzia ngazi za
matawi, kata, wilaya na mkoa.
Alitaja kazi zingine alizozifanya ni kufanya ziara tofautitofauti na
viongozi mbalimbali wa kitaifa waliofika mkoani hapa kama Daniel Chongolo, Mary
Chatanda na Rais Samia Suluhu Haasan na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Gwau alitaja mambo mengine aliyofanya ni uchangiaji wa shughuli za
maendeleo kama ujenzi wa miundombinu.ujenzi wa nyumba za makatibu wa chama
katika wilaya tano kwa awamu ya kwanza na kuwa Wilaya ya Manyoni hakuweza
kuchangia kutokana na eneo la ujenzi kuwa na mgogoro ambapo alisema atatoa
mchango mwingine kwa awamu ya pili wakati wa ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba
hizo.
Aidha, Gwau alisema kazi nyingine aliyoifanya ni kushiriki kuwaingiza
wanachama wapya wa UWT kwa kutoa kadi 2500 kwa awamu ya kwanza kwa mwaka 2023
na kuwa kwa mwaka 2024 atafanya hivyo tena lengo likiwa ni kuwa na wanachama
wengi watakaokisaidia chama.
Alitaja kazi nyingine aliyoifanya ni kufanya ziara ya kupita kila kata japo
si kwa asilimia 100 lengo likiwa ni kuonana na viongozi wa jumuiya ya wanawake
ambao wanazijua changamoto zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuzingatia kuwa wao
ndiyo wamepewa dhamana ya uongozi na kuwa alipokea asilimia 95 za changamoto.
Alizitaja baadhi ya changamoto alizozipokea kuwa ni kutokuwa na vifaa vya
kufanyia kazi, matawi yao kuwa mbali na kata, kutokuwa na sare ambapo pia
walibainisha changamoto za miundombinu ya barabara, maji na umeme.
"Nikiwa mbunge nilifanya ziara hiyo kwa lengo la kujua maeneo na
miundombinu na kupata fursa ya kukutana na madiwani wa maeneo husika ambao
walinieleza changamoto zilizopo na ziara hii niliifanya kwa miezi minne kwa
mkoa wote," alisema Gwau.
Alisema jambo lingine alililolifuatilia ni mikopo ya asilimia nne kwa
wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa walemavu ambayo
ilisimamishwa na Serikali na kuwa amekuwa akifuatilia kujua lini itarejeshwa na
kutakuwa na vigezo gani kwa ajili ya kuipata.
Gwau alisema changamoto zingine alizozipokea katika ziara zake hizo ni
kutokuwa na uwanja wa ndege wa uhakika mkoani hapa, kushuka kwa bei ya zao la
alizeti, miundombinu ya barabara, umeme, maji na zile zilizohusu sekta ya
elimu.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Singida, Martha Mayaga akizungumza kwenye mkutano
huo wakati akitoa salamu za chama aliishukuru Serikali chini ya Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo na akaomba jitihada hizo zinazofanywa na Rais zinapaswa kuungwa mkono
na kila mpenda maendeleo.
Mayaga aliwataka wanawake hao kuwa na umoja na kushirikiana katika kila
jambo na kukifanya chama hicho kiendelee kushika kutawala nchi.










No comments:
Post a Comment