TANGA KUNUFAIKA MRADI MKUBWA WA MAJI MIJI 28 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, 26 December 2023

TANGA KUNUFAIKA MRADI MKUBWA WA MAJI MIJI 28

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM),Mhandisi Yohana Stephen Mgaza.akizungumzia mradi huo. 

.........................................

 Na Mashaka Kibaya, Tanga.

 

KOROGWE Mji, Handeni, Pangani na Muheza ni maeneo ambayo Wananchi wake watanufaika na Mradi mkubwa wa Maji unaofahamika kama Mradi wa Miji 28.

Mradi wa Maji wa Maji wa Miji 28 unaotarajiwa kuyekelezwa hapa nchini Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi ili kuwaondoshea kero kwa Wananchi wake.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipata mkopo nafuu kutoka Serikali ya India Kiasi cha Dola 500 Milioni zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Maji wa Miji 28 nchini.

Aidha Mamlaka ya Maji Safi Handeni Trunk Main (HTM) ni sehemu ya utekelezaji Mradi wa Miji 28 ambapo watatekeleza mradi utakaohudumia Miji mine ya Handeni,  Korogwe, Muheza na ule wa Pangani.

Yohana Stephen Mgaza ni Mhandisi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Handeni Trunk Main (HTM) Wilayani Handeni.

Katika mazungumzo yake na Mwandishi wa Makala haya, Mhandisi Mgaza alisema kwamba, kwa upande wa Korogwe, Handeni, Pangani na Muheza Mradi utagharimu dola 81 Milioni ambazo ni zaidi ya Shilingi 200 Billioni hadi mradi kukamilika.

"Ni mradi mkubwa ambao tunategemea kuusimamia kwa makini ,ni fedha nyingi sana ya Serikali itatumika"alisema Mgaza huku akibainisha kuwa mradi huo utakuwa na chanzo kimoja ambacho ni Mto Pangani.

Kutoka Mto Pangani Maji yatachukuliwa kwenye eneo la Kijiii cha Mswaha Darajani, yatasafirishwa mpaka Kijiji cha Tabora kutakakojengwa mtambo wa kisasa kuchuja Maji.

Baada ya hapo ndipo Maji yatatawanywa kwenda maeneo mbalimbali katika Miji ya Handeni, Korogwe, Pangani na Muheza kutakakojengwa matenki makubwa kwa ajili ya kuhifadhia Maji hayo.

Katika Mji wa Handeni tenki lenye ujazo wa lita Milioni mbili litajengwa, Muheza tenki la lita milioni mbili, Pangani kutajengwa matenki ya ujazo lita 500,000 Kijiji cha Boza,lita 300,000 Kijiji cha Madanga na tenki jingine la lita laki mbili kujengwa kwenye Kijiji cha Ubangaa.

Mradi wote huo urefu wake ni Kilomita 189 kutoka kwenye Chanzo mpaka kufikia maeneo ya matenki ambayo yanakwenda kuwahudukia Wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa HTM (Mgaza) alisema kwamba, kwa kuanzia yatajengwa mabomba ya kusambaza maji kwenye urefu wa Kilomita 100 maeneo yote ya Miji na baadaye kazi ya uaambazaji maji kwa Wananchi itaendelea.

M/s JWIL Infra Construction Limited ndiye Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo akisimamiwa na Mtaalam Mshauri Kampuni ya Wapcos zote za kutoka nchini India.

HTM inabakia kuwa Wataalam wa Wizara ya Maji wakiwa Wasimamizi kuhakikisha mradi unajengwa kwa viwango ambavyo umefanyiwa Usanifu kazi ambayo Mhandisi Yohana Mgaza ameahidi kuitekeleza.

Mradi huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya Watu 600,000 kwenye Miji hiyo ya Pangani, Korogwe, Muheza na Handeni huku Wananchi watakaokuwa Vijiji vilivyo umbali wa Kilomita 12 kutoka bomba kuu popote litakapokuwa linapita wakitarajiwa kunufaika.

Tayari mkabdarasi yuko eneo la Mradi anaelezwa kuendelea na kazi akilaza mabomba kwenye maeneo mbalimbali ambapo kuna kipande cha kutoka tenki la Korogwe kielekea Tabora kwenye Chujio alikoanza kulaza bomba.

Pia mkandarasi ameanza kulaza bomba kutoka Kijiji cha Komsala kuelekea Kijiji cha Mandela na kutoka Mandela kuelekea kwenye Kijiji cha Masatu.

Vilevile mabomba mengine yamelazwa kwenye Kijiji cha Tabora kuelekea Mji wa Korogwe huku ujenzinwa matenki ukiwa umeanza na yaliyopo hatua ya kukwaga zege ni lile la Kijiji cha Madanga na Boza wilayani Pangani.

Kwingine kazi ya kusafisha maeneo inaendelea ili ujenzi kuanza rasmi huku ujenzi ukitarajiwa kuanza tenki la Vibaoni Handeni na kusafisha eneo la kujenga Chujio Tabora.

Usafishaji unaendelea eneo la kujenga Chanzo Mswaha ambapo kazi inaendelea vizuri ambapo Mhandisi Yohana Mgaza anaishukuru Serikali ya awamu ya Sita kufikia malengo ya kupata fedha za kutekeleza mradi utakaonufaisha Wananchi walio wengi.

Pongezi nyingine zinakwenda kwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa juhudi zake za kuhakikisha mradi unafanyika ambapo Wataalam wa HTM wameahidi kutokuwa kikwazo na mradi utajengwa kwa viwango stahiki.

"Sisi kama Wataalam wa HTM tukiwakilisha Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo, tutahakikisha mradi unajengwa kwenye viwango stahiki na kukamilika kama ulivyopangwa"alisema Mhandisi huyo wa HTM.

Mgaza hakusita kuzungumzia suala la usiirikishwaji Wananchi kwenye Mradi akisema,kabla utekelezaji kuanza walishirikiana na Viongozi wa vijiji, kata tarafa Chama na Serikali kupita maeneo yatakayoguswa na mradi.

Uhakiki wa Wananchi wenye maeneo yenye mazao umefanyika ili kufidiwa na kusikokuwa na mazao wameombwa ili kuweza kufanikisha kufika kulikokusudiwa.

Mradi huo ulioanza Aprili 2023 unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba 2024 ingwa awali ilikuwa iwe Disemba 2025 ambapo unafanyika kwa njia ya Usanifu na ujenzi.

Hayo yamejiri baada ya kuonekana umuhimu na mahitaji makubwa kwenye maeneo ya wananchi ambapo HTH iliketi na wataalam washauri na wakandarasi kupitia mpango kazi wa utekelezaji na hivyo kujiwekea malengo.

Mradi huo wa Miji 28 kwa Wilaya za Handeni, Pangani, Korogwe na Muheza unaonekana kuwa fursa ya kujikwamua kiuchumi kwa wananchi kwenye maeneo kazi zitakakofanyika.

Kipaumbele kutatolewa jwa wenyeji kushiriki shughuli za mradi ambapo vijana wamehamasishwa kujitokeza huku Mhandisi Yohana Mgaza akisema akina Mama pia wanaweza kujitokeza kwa biashara ya chakula. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad