NA DOTTO MWAIBALE
MKOA wa Singida unatarajia kuanzisha mfuko wa elimu kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaofanya vizuri kimasomo lakini wanashindwa kuendelea na shule kutokana na wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwasomesha.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameonesha nia ya kuanzisha mfuko huo wakati akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichoketi Disemba 15, 2023 katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida ambacho kilikuwa na agenda zaidi ya tisa.
"Tukitaka watoto wetu wafanye vizuri na ufaulu uongezeke ni lazima tuanzishe mfuko wa elimu wa Mkoa wa Singida ambao utakuwa ukiwasaidia wanafunzi ambao wanafanya vizuri lakini wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha,"alisema Serukamba.
Serukamba alisema utaratibu wa kuwabaini wanafunzi hao ambao wazazi wao hawana uwezo utafanyika kuanzia kwenye maeneo wanayoishi kupitia viongozi mbalimbali wakiwemo watendaji wa vijiji na walimu wakuu wa shule.
Aidha, Serukamba alitaja mambo kadhaa ambayo yataweza kuongeza ufaulu wa watoto kuwa ni kufanyika vikao vya mara kwa mara na maafisa elimu kata kwa kusimamiwa na mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, maafisa elimu, diwani na watendaji wa kata, wakuu wa wilaya kufuatilia utoro wa wanafunzi kuanzia shuleni hadi nyumbani kwao, upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wakiwa shuleni.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga akichangia kuhusu mpango huo aliuunga mkono na kueleza kuwa unawezekana kwa asilimia 100 akitolea mfano wa Wilaya ya Bahi iliofanikiwa katika jambo hilo.
"Jambo hili linafanyika pale Bahi na fedha zinapatikana kupitia vibali vya mifugo ambayo ilikuwa inaleta mapato karibia asilimi 60 katika minada ambapo kwa kila ng'ombe ilikuwa ni Sh.2000 lakini ili kuufanya mfuko huo uwe na fedha waliptisha kwenye baraza la madiwani iwe Sh.4000 ambapo Sh.2000 iliyoongezwa ilikuwa ikienda moja kwa moja kwenye mfuko wa elimu na kuwa chanzo kikubwa cha kuingiza hela kwenye mfuko huo," alisema Mganga.
Alisema baada ya kupata fedha hizo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo alikuwa akipita kwenye vijiji na kata kuwa ambia wananchi kuwa hawana shida ya kuwapeleka watoto shule kutokana na kuwa na mfuko huo wanachohitaji ni mtoto afaulu na wampeke kwao ili waweze kumnunulia mahitaji yake ya shuleni jambo ambalo liliwaibua baadhi ya wazazi wakisema wanawatoto ambao wamefaulu lakini hawapo shuleni kwa kukosa mahitaji.
Alisema Singida nao wanaweza kuangalia moja ya chanzo cha mapato ambacho ni kizuri nao wakafanya kama walivyofanya Wilaya ya Bahi na kuwa fedha hiyo itakuwa ikiwasaidia watoto wa wilaya husika na sio nje ya hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleimani Mwenda, akichangia jambo kwenye kikao hicho alisema hivi sasa kumekuwa na changamoto kubwa ya kesi za kupata mimba kwa wanafunzi wa sekondari na msingi jambo ambalo linasababisha wanafunzi wengi kukatisha masomo yao.
Alisema mbali ya mimba suala la ulawiti limekuwa ni tishio mashuleni akitolea mfano kwenye wilaya yake ambapo baadhi ya watoto wamekuwa wakiwalawiti wenzao na hata wanapofikishwa polisi au mahakamani wamekuwa wakiruka dhamana na kukikimbilia maeneo mengine ambako nako wamekuwa wakirudia kufanya vitendo hivyo.
Alisema baadhi ya watuhumiwa hao wa ulawiti wamekuwa hawaogopi kufanya matukio hayo na wamekuwa wakitembea na mafuta ya bei kubwa (vilainishi) jambo ambalo linatia mashaka kuwa huenda nyuma ya mambo hayo kuna nguvu ya ziada inafanyika na kuwa ameunda kamati ya kufuatilia jambo hilo ili kubaini kiini cha matukio hayo ambayo yamekuwa ni mengi katika wilaya hiyo.
Baadhi ya agenda zilizojadiliwa katika kikao hicho ni utekelezaji wa bajeti ya 2022/ 2023, mapango na bajeti ya 2023/2024, utekelezaji wa bajeti kipindi cha Julai-Oktoba 2023, Hali ya huduma za elimu na afya, hali ya chakula na mikkati ya kilimo, utabiri wa mvua 2022/2023 na 2023/ 2024.
Agenda nyingine zilikuwa ni hali ya upatikanaji wa maji safi na salama, hali ya upatikanaji wa umeme, wasilisho kutoka ofisi ya Takwimu ya Taifa na wasilisho kutoka TIRA.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga akichangia kuhusu uanzishwaji wa mfuko wa elimu wa Mkoa wa Singida.
Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Singida wakiwa kwenye kikao hicho.














No comments:
Post a Comment