(NA MPIGAPICHA WETU)
---------
Na Mwandishi Wetu, Chato- Geita
MKUU wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella amehimiza
jamii kujenga utamaduni endelevu wa kupanda miti kwani kwa sasa ni fursa ya kibiashara
inayolenga kukuza kipato cha kaya, familia na taifa kwa ujumla.
Mhe. Shigella ametoa rai hiyo tarehe 1 Juni, 2024 Wilayani
Chato Mkoani humo wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika
eneo la Hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kilele
cha Siku ya Mazingira Duniani itayofanyika tarehe 5 juni mwaka huu.
Mhe. Shigella amesema uhifadhi wa mazingira inaenda sambamba
na zoezi la upandaji miti ambapo kwa sasa kumebua fursa ya biashara ya kaboni
na hivyo kuhimiza jamii kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao ili kuweza
kujiongeza kipato.
Ameeleza kwa sasa mti ni fursa ya kibiashara kwani
ukipandwa na kustawi unaongeza kipato kupitia kaboni na kuwataka wananchi kuchangamkia
fursa hiyo ambayo pia itatimiza dhamira ya kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka
katika kila halmashauri inafikiwa na kuhimiza wajibu kwa viongozi na watendaji
wa Serikali kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo.
Kwa mujibu wa Shighella ameeleza kuwa suala la
upandaji miti kwa sasa limepewa msukumo na kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita
ambapo kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeandaa kanuni na miongozo ya
usimamizi wa biashara ya kaboni inayolenga kuwanufaisha wananchi.
Amefafanua kuwa ili kufikia malengo ya upandaji miti ni
wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anajenga utamaduni wa kupanda miti katika
maeneo ya makazi, ikiwemo nyumba za ibada, maeneo ya masoko, vituo vya afya n.k.
Aidha Shighella ameeleza kuwa kutokana na fursa
zilizopo kupitia kaboni, Mkoa huo upo mbioni kuandaa mkutano wa wadau wa
mazingira ikiwahusisha viongozi wa serikali na wawakilishi wa wananchi ili
kujadiliana mbinu na mikakati inayolenga kuwanufaisha wananchi.
Pia Mhe. Shighella amewasihi wananchi kuachana na
shughuli zisizo endelevu ikiwemo uchimbaji holela wa madini ambao umekuwa ukisababisha
athari kwa mazingira ikiwemo ukataji miti na kuwahimiza wasimamizi wa maeneo ya
migodi kuhakikisha wanapanda miti ili kurejesha na kutunza uoto wa asili.
“Tuna wajibu wa kurejesha na kutunza uoto wa asili uliopo
nchini kwani utunzaji wa mazingira ni jambo
muhimu linalobeba mustakabali wa maisha ya vizazi vya sasa na vijavyo sambamba
na kutunza mifumo ekolojia iliyopo majini na ardhini” amesema Shigella.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi
Cyprian Luhemeja ameupongeza Mkoa wa Geita kwa juhudi mbalimbali inazoendelea
kuzifanya katika kusimamia masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira
ikiwemo usafi na upandaji miti.
Ameongeza kuwa uwepo wa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi
umeibua fursa ya kipato na kiuchumi kwa jamii kupitia kaboni inayotokana na
faida ya upandaji miti, ambapo kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeweka
mazingira wezeshi kwa kuandaa kanuni na miongozo ya usimamizi wa biashara hiyo.
Mhandisi Luhemeja amesema ili kuhakikisha jamii
inanufaika na fursa zilizopo katika kaboni, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa
viongozi wa serikali za mitaa, wabunge na makundi mbalimbali wakiwemo
wawekezaji.
“Miti kwa sasa ni biashara hivyo kutokana na umuhimu uliopo,
Serikali inahamasisha biashara ya kaboni……Kuelekea Siku ya Mazingira Duniani
Juni 5 mwaka huu tutatoa hundi ya shilingi Bilioni 14 kwa halmashauri ya
Tanganyika, Mkoani Katavi ambayo inafanya biashara hii” amesema Mhandisi
Luhemeja.
Nae Mbunge wa Chato, Mhe. Medard Kalemani ameishukuru
Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuichagua Wilaya hiyo kuongoza shughuli za usafi wa
mazingira katika Mkoa wa Geita na kueleza viongozi na watendaji wamejipanga
vyema kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali ya kupanda miti na kusimamia
usafi wa mazingira.
“Wilaya ya Chato tumejiwekea mkakati kwa kuhakikisha
tunapanda miti isiyopungua 1000 kwa mwaka ili kutunza mazingira na tayari tuna
msitu wa Silayo ambapo hadi sasa tumepanda miti ekari 98,000 na miti yote ipo
katika hali nzuri na inaendelea kutunzwa” amesema Mhe. Kalemani.
Tarehe 5 Juni ya kila mwaka Tanzania huungana na Jumuiya ya Kimataifa katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Kauli Mbiu ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2024 inasema
“Urejeshwaji wa Ardhi, Ustahimilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame”









No comments:
Post a Comment