Rai hiyo imetolewa hapo jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wà Morogoro, ambaye ni
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini Mhe. Rebeka Nsemwa, wakati akifungua kikao
kazi cha wateja na wadau wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, kilichokutanisha
viongozi wa sekta ya afya ngazi ya mkoa na wilaya mkoani humo.
_“Mkoa huu una jumla vya vituo 378
vya kutolea huduma za afya ambavyo vinajumuisha hospitali kumi na sita(16),
ikiwemo hospitali mbili za rufaa, vituo vya afya arobaini na sita (46) na
zahanati mia tatu kumi na sita (316), hivyo fanyeni kazi kwa pamoja na
kujadiliana namna bora ya kuboresha utekelezaji wa majukumu yenu, na hata
kupeana mrejesho wa masuala mbalimbali yanayohusiana na mnyororo wa ugavi wa
bidhaa za afya.” Alisisitiza Mhe. Nsena
Mhe. Nsemwa amewataka viongozi hao kuhakikisha wanakuwa na majadiliano
yenye tija kwa kuainisha namna bora ya kufanya kazi kwa pamoja, badala ya
kutupiana lawama na kunyosheana vidole, ili kila upande uweze kutimiza wajibu
wake katika kuwahudumia wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Nsemwa amewataka watendaji hao kuboresha maoteo
yao ya bidhaa za afya, kwenye vituo wanavyosimamia kila mmoja katika eneo lake,
ili kuepukana na sintofahamu ya ukosefu wa bidhaa za afya vituoni,
inayosababishwa na taarifa zisizosadifu mahitaji halisia.
Watalamu hao wa afya pia wametakiwa kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za
afya, kwa kila mmoja ana wajibu wa kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za afya,
ili kuleta tija kwa wananchi, kwani serikali imekuwa ikiongeza na kutenga
bajeti ya dawa na vifaa tiba ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Aidha, Mhe. Nsemwa amewahimiza watendaji hao kulipa na kupunguza madeni yao
wanayodaiwa na MSD, ili kuiongezea MSD uwezo wa kuwahudumia wateja wake,
kutokana na vituo hivyo vya kutolea huduma za afya, kuwa na limbikizo la
madeni, hivyo kuathiri utendaji wa MSD.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amewasilisha mchakato
wa maboresho mbalimbali ya huduma za MSD, kwa kuainisha hatua mbalimbali
zilizofikiwa kwenye maboresho ya huduma, na utendaji,huku akiahidi kufanyia
kazi yale yote yaliyoibuliwa ndani ya kikao hicho ili kwa pamoja kuweza
kuboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
Tukai pia ameainisha jinsi MSD ilivyojikita katika mchakato wa uanzishaji
wa viwanda mbalimbali vya bidhaa za afya nchini, mathalani viwanda vya barakoa,
mipira ya mikono,na viwanda vya bidhaa za pamba ili kuondoa utegemezi wa bidhaa
kutoka nje ya nchi.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es salaam, Betia Kaema, amewashukuru Wadau
hao kwa kuitikia wito na kuhudhuria kikao hicho kwani imeonyesha ni jinsi gani
wadau hao walivyo na kiu ya kuboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya
mkoani humo, hivyo kuahidi kuchukua ushauri na maoni yao ili kuboresha utendaji
wa Kanda hiyo.
Taswira ya mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai akizungumza kwenye mkutano huo.
Mdau wa MSD wakikabidhiwa cheti cha kushiriki mkutano huo.









No comments:
Post a Comment