JESHI LA POLISI MKOA WA TANGA LAJIDHATITI ULINZI WA RAIA NA MALI ZAO - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, 27 September 2025

JESHI LA POLISI MKOA WA TANGA LAJIDHATITI ULINZI WA RAIA NA MALI ZAO

 Lawatoa hofu wanahabari, kuhusu usalama wao wakiwa kazini.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa  Tanga,  Almachius Mchunguzi akizungumza na waandishi wa habari Septemba 26, 2025 katika mdahalo kuhusu ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari kuelekea uchaguzi mkuu.

.....................................

Na Mashaka Kibaya,Tanga.

KATIKA kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani hapo Oktoba 29 mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoani Tanga limejipanga kikamilifu kutoa ulinzi wa kutosha kwa makundi yote wakiwemo waandishi wa habari ambapo limewasihi wanatasnia hao kutekeleza majukumu yao kwa haki. 

Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga Almachius Mchunguzi ameyasema hayo jana katika mdahalo kuhusu ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari kuelekea uchaguzi mkuu akisema,kwa Mkoa wa Tanga hali imeendelea kuwa shwari na jeshi la polisi limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia pamoja na mali zao.

Katika mdahalo huo wa wadau ulioandaliwa na klabu ya Waandishi wa habari wa Tanga TPC, muungano wa klabu za wanahabari nchini UTPC na shirika la kimataifa la International media support, mgeni rasmi alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga Almachius Mchunguzi. 

Katika hotuba yake,Kamanda Mchunguzi mbali na kuwatoa hofu wanahabari kuhusu usalama wao watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao katika kipindi hiki cha uchaguzi,aliwasihi kufanya kazi zao kwa kuzingatia msingi ya haki,sheria, miiko na maadili ya tasnia hiyo ya habari. 

Aidha Mchunguzi alisema, wanahabari wanapotekeleza majukumu yao ni vyema wakazingatia utaifa kwa kuepuka kuandika mambo yatakayosababisha uchochezi utakaoleta uvunifu wa amani.

" Ni vyema habari mnazozitoa zikazingatie utaifa, uchochezi utakaochangia uvunifu wa amani usifanyike katika uandishi wa habari, jukumu la kulinda amani ni kwa wote "alisema kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Mkoani Tanga. 

Lulu George ni Mwenyekiti wa klabu ya Waandishi wa Habari Mkoani Tanga (TPC), katika mazungumzo yake alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye mdahalo huo.

Mwenyekiti huyo wa TPC alielezea kuridhishwa kwake kwa mahusiano mazuri yaliyodumu kwa kipindi kirefu baina ya waandishi wa habari na jeshi la polisi, alisema hali hiyo inapaswa kudumishwa. 

Kuhusu mdahalo huo Lulu aliwataka washiriki, kufanya majadiliano ya wazi kwenye changamoto hususani zinazowakumba wanahabari wakiwa kazini, alisisitiza umuhimu wa kujua mipaka yao ya kazi kwa kuzingatia wajibu pamoja na haki za wengine.

Katika mdahalo huo wadau walioshiriki ni Waandishi wa Habari wa mkoa wa Tanga, viongozi wa dini,jeshi la polisi na wadau kutoka vyama vya siasa pamoja na wanasheria ambapo mada zilizowasilishwa ni nafasi ya jeshi la polisi katika ulinzi na usalama wa Waandishi wa habari, sheria na haki za waandishi wa habari nchini Tanzania na uzoefu wa madhila kwa wanahabari.

Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Tanga,  Lulu George.akizungumza kwenye kongamano hilo.
Waandishi wa habari Mkoa wa Tanga wakiwa kwenye kongamano hilo.
Washiriki wa kongamano hilo wakiwa katika picha ya pamoja 
Wadau mbalimbali walioshiriki kongamano hilo wakiwa katika picha ya pamoja.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad