POLISI TANGA YAWATIA MBARONI WALIOFANYA UTEKAJI KUJIPATIA FEDHA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, January 28, 2026

POLISI TANGA YAWATIA MBARONI WALIOFANYA UTEKAJI KUJIPATIA FEDHA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP),  Almachius Mchunguzi, akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya matukio mbaalimbaali Januari 27, 2026.

........................

Na Dotto Mwaibale 

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa  kuwatia mbaroni watuhumiwa wawili, Steven Elia (27) mkazi wa Moshi na Moses Joseph (Maarufu Kisoko)  (26) mkazi wa Tanga kwa kosa la utekaji ili wajipatie fedha. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP),  Almachius Mchunguzi akielezea tukio hilo Januari 27, 2026 alisema kuwa Januari 6, 2026, Halidi Ramadhani aliripotiwa kutekwa na watu waliokuwa wakiwasiliana na familia yake wakitaka wapewe Sh. Milioni 14. 

“Januari 19, 2026 majira ya saa 3 asubuhi, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao waliokuwa wakimshikilia mtu huyo kinyume cha sharia na tayari wamefikishwa Wilaya ya Handeni kwa hatua za kisheria ,” alisema. 

Katika matukio mengine jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata vijana waliokuwa wakijihusisha na uporaji wa simu na kuwajeruhi wananchi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Tanga. 

Akizungumza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa operesheni za mwezi Januari 2026, Kamanda Mchunguzi alisema kuwa katika kudhibiti wimbi la uporaji wa simu, jumla ya simu 60 zimekamatwa, kati ya hizo simu 35 zimetambuliwa na kurejeshwa kwa wamiliki wao huku simu 25 zikiendelea kuhifadhiwa kituoni kwa ajili ya utambuzi na taratibu nyingine za kisheria. 

“Jeshi la Polisi limeendelea kuchukua hatua kali dhidi ya vijana wanaojihusisha na uporaji wa simu na kuhakikisha usalama wa wananchi unarejea,” alisema ACP Mchunguzi. 

Mchunguzi alisema katika kipindi hicho hilo  limefanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 55 wa makosa mbalimbali, wakiwemo watuhumiwa tisa waliohusika katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha za jadi aina ya mapanga na kuiba pikipiki.

Alitaja makosa waliyoyadhibiti kuwa ni pamoja na wizi, uporaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, makosa ya usalama barabarani na makosa ya kimaadili. 

Alisema katika operesheni hizo pia pikipiki 50 zimekamatwa kwa tuhuma za kuhusishwa na uhalifu, ambapo pikipiki 28 kati ya hizo hazikuwa na namba halali za usajili. Aidha, mali mbalimbali zilizodhaniwa kuwa za wizi zimekamatwa zikiwemo runinga saba, friji moja, magodoro matatu pamoja na madumu 26 ya mafuta ya dizeli. 

ACP Mchunguzi alisema jeshi hilo linamshikilia Ally Ramadhani maarufu Ally Bwengo (38), fundi welding mkazi wa Amboni-Tanga, kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha lililotokea Agosti 19, 2025. 

Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela lakini alitoroka kutoka Gereza la Maweni, kabla ya kukamatwa tena baada ya ufuatiliaji wa kina. 

Katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ACP Mchunguzi alisema kilo 104 za mirungi na kilo 24.6 za bangi zimekamatwa. Aidha, mtuhumiwa Mkombozi Masimiusi (40), mkazi wa Dar es Salaam, alikamatwa wilayani Korogwe akiwa na vipande 19 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 52 na tayari amefikishwa mahakamani. 

Kwa upande wa makosa ya kimaadili, Kamanda huyo alisema wilayani Pangani, Said Ramadhan Said maarufu Mbezi (23) alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kulawiti, huku wilayani Korogwe watuhumiwa wawili wakihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kwa kosa la kupatikana na nyara za serikali. 

Vilevile, watuhumiwa wawili wa shambulio la aibu wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela. 

ACP Mchunguzi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu ili jeshi hilo liweze kuwakaamata ili sharia iweze kuchukua mkondo wake. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad