.................................
Na Mwandishi Wetu.
WAFUGAJI wa jamii ya kimasai, wanadaiwa kuwashambulia na kuwakata mapanga baadhi ya wakulima wa Kijiji cha Mbwade, Kata ya Mandoto Tarafa ya Kimamba, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Tukio hilo lililotokea Januari 14, mwaka huu, inadaiwa mkazi wa Mbwade, Kibibi Mohamed mwenye umri wa miaka 71 alijeruhiwa kwa kukatwa na panga sehemu ya jicho. Katika tukio hilo, Salum Mkude mwenye umri wa miaka 34, alijeruhiwa mkononi baada ya kutokea ugomvi mkubwa na jamii ya wafugaji wa kimasai.
Akizungumza kutoka Morogoro kwa njia ya simu, mkazi wa kijiji hicho, Yusuf Ngomangira, alisema tukio hilo lilitokea saa 6 mchana, baada ya wafugaji wa kimasai kutaka kulisha ng'ombe wao katika shamba la wakulima hao.
Ngomanjira ambaye ni mama mzazi wa Kibibi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Mbwade alisema wakulima hawana amani kutokana na kushambuliwa mara kwa mara na wafugaji.
Alisema baada ya tukio hilo, walimpeleka Kibibi Kituo cha Polisi cha Kimamba na kupatiwa PF3 kwa ajili ya kwenda kutibiwa katika hospitali ya Kimamba.
Alisema kutokana na ukubwa wa jelaha lake, Kibibi aiishonwa nyuzi tatu na anaendelea na matibabu.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema pamoja na tukio hilo kuripotiwa polisi, lakini hadi sasa watuhumiwa hawajakamatwa ili wakifikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Ngomangira alisema anashindwa kufahamu kwa nini watuhumiwa hao hawajakamatwa ambao wanajulikana kwa majina.
Alisema wakulima wanapata tabu kutokana na mamlaka ya serikali ya kijiji hicho ipo chini ya uongozi wa jamii ya kimasai.
Pia alisema viongozi hao wanatengeneza kuonekana wakulima hawana haki katika ardhi hiyo.
Alisema ugomvi wa wakulima na wafugaji ulianza mwaka 2001, baada ya jamii hiyo ya kimasai kuhamia katika kijiji hicho na maeneo mengine ya Kilosa.
Hata hiyo, Diwani wa Kata ya Mandoto, Ashura Changula, alikiri kutoka kwa tukio hilo.
Diwani huyo alisema walishuhudia tukio la Kibibi na Mkude alijeruhiwa na jamii ya kimasai na kuripotiwa polisi Kata.
"Ni kweli tukio hili limetokea na polisi kata wanalifahamu," alisema Ashura.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alikataa kuzungumzia tukio hilo.
"Siwezi kutoa taarifa yoyote mpaka ufike ofisini," alisema Mkama.







No comments:
Post a Comment