CCWWT CHAJIPANGA KWA MKUTANO MKUU, KUOMBA SHERIA YA KUWATAMBUA KUPATA MIKOPO YA ASILIMIA 10 - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, 22 February 2026

CCWWT CHAJIPANGA KWA MKUTANO MKUU, KUOMBA SHERIA YA KUWATAMBUA KUPATA MIKOPO YA ASILIMIA 10

Rais wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania (CCWWT), Tadey Mchena akizungumza na wanachama wa chama hicho Februari 21, 2026 Jijini Arusha.

.......................................

Na Hamida Kamchalla, Arusha


CHAMA cha Wazee Wanaume Tanzania (CCWWT), kinajipanga kufanya mkutano wao mkuu wa kwanza tangu kuanzishwa kwake ajenda kubwa ikiwa ni kuomba itungwe sheria ya kuwatambua ili waweze kupata mikopo ya asilimia 10 kama wanavyopata wanawake, vijana na watu wenye ulemavu..

Hayo yalijiri katika kikao kilichoketi Februari 21, 2026 kwa ajili ya kupanga maandalizi na mikakati kuelekea mkutano mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu jijini Dodoma.

Katika kikao hicho wamewaomba wadau mbalimbali kuwaunga mkono ili kufanikisha maandalizi ya mkutano huo ambao utawaibua wazee wengine kujiunga na chama hicho ambacho ni cha umuhimu kwa kuwaweka katika jukwaa moja..
 
Rais wa CCWWT, Tadey Mchena alisema lengo kubwa la mkutano huo ni kufanya majadiliano ya katiba ya chama chao na mambo mengine kadha wa kadha na kuona namna ya kuweza kuwaingiza wanawake wazee kwenye chama hicho.

Mchena alisema sambamba na hayo wanamuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan iundwe sheria rasmi ya kuwatambua wazee wanaume kama ilivyo wanawake, vijana na wenyewe mahitaji maalumu kupata mikopo ya asilimia 10.

"Tunaliomba hili na sisi tuweze kupata mikopo ya asilimia 10, kwa sababu tayari tuna miradi yetu, lakini pia tunaomba tuwe na mwakilishi wetu  bungeni na katika vyombo vya maamuzi kama ilivyo kwa makundi mengine" alisema.

Naye Mwenyekiti wa CCWWT Mkoa wa Arusha, Christopher Mollel alisema wamejipanga na kufuatilia sana mkutano huo hivyo wamewaomba wadau ili kufanikisha kwani wanaamini utakuwa wa kitaifa kwakuwa viongozi wa ngazi za juu wa chama na Serikali watahudhuria..
 
Mollel ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa CCWWT  alisema chama hicho kina nguvu na tayari wamefikia hatua ya kuwafuata wazee wa vijijini hususani wasiojiweza ili kuwaenzi na kuwafariji ili kuwapa tumaini la kuishi badala ya kuwa wapweke..

"Hii Ina maanisha kinafanikisha malengo ya wazee, tumejipanga kuwasemea wazee juu ya changamoto wanazokabiliana nazo kwani baadhi yao ni wagonjwa na kupata tiba kwao ni ngumu, lakini kupitia chama chetu tukipaza sauti wanaweza kupata unafuu wa kutibiwa" alisema Mollel.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Afya CCWWT, Dk. Nsiande Urasa alisema kati ya mengi chama hicho kimelenga kuhakikisha wazee wanaangaliwa kwa ukaribu hasa katika suala la afya, hususani bima zao za afya zinalipwa kulingana na Sera ya wazee ya mwaka 1973 ambayo imefanyiwa maboresho mwaka 2024.

"Sera hii inazungumzia tiba na matibabu jumuishi kwa wazee, tumeona wazee wengi wamepata changamoto mbalimbali za kiafya, hususani magonjwa sugu,

Ningependa kutoa rai kwa Serikali kutoa kibali maalumu kwa ajili ya wazee kama ilivyofanya kwa mama na mtoto, kwani nao wametumikia Taifa hili hivyo na wao waweze kunufaika kwa namna moja au nyngine" alisema Dk. Urasa.
 
Yusuph Dachi  Katibu wa CCWWT, Wilaya ya Arusha mjini alisema hata wazee waliokuwa vijana zamani na waliishi kwa amani na umoja pasipo vurugu wala migogoro baina yao na Serikali.


Dachi aliongeza kuwa sasa chama hicho kina miradi ya kilimo, wana shamba la heka 10 maeneo ya Lokii, pamoja na ufungaji wa nyuki katika kilima cha Sule eneo la Kijenge ambapo wana mizinga zaidi ya 50 ya nyuki wadogo.

Wanachama wakiwa kwenye kikao hicho. 

 Wanachama wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao hicho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad