KAMATI YA LAAC YATOA MAELEKEZO YA KUBORESHA MIRADI YA MAENDELEO JIJINI MWANZA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 25 March 2026

KAMATI YA LAAC YATOA MAELEKEZO YA KUBORESHA MIRADI YA MAENDELEO JIJINI MWANZA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imekamilisha ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, ambapo imetoa ushauri na maelekezo yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa fedha na ukamilishaji wa miradi hiyo.

Akizungumza

Machi 24, 2026, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Ado Shaibu, amebainisha maeneo kadhaa yanayohitaji marekebisho ili kuendana na matakwa ya kisheria na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kuhusu mradi wa ujenzi wa majengo ya Idara ya Afya, Kamati imemuelekeza Afisa Masuuli kuhakikisha kiasi cha shilingi 527,049,323 kilichotolewa kama malipo ya awali kwa mkandarasi kinarejeshwa. Aidha, Kamati imetaka kuwepo kwa uthibitisho wa mapokezi ya fedha hizo kwa CAG kila robo mwaka kwa ajili ya uhakiki.

Vilevile, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeombwa kupitia upya taratibu zilizotumika katika malipo ya shilingi 1,125,678,889 na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria kwa watumishi waliohusika na ukiukwaji wa kanuni za manunuzi.

Katika mradi wa Soko Kuu la Mwanza, Kamati imesisitiza umuhimu wa kukamilisha miundombinu ya msingi kama mifumo ya maji nje ya soko na ufungaji wa kamera za usalama (CCTV). Maelekezo hayo yanalenga kuimarisha ufanisi na usalama wa soko hilo kwa manufaa ya wafanyabiashara.

Pia, uongozi wa Jiji umepewa hadi tarehe 30 Mei, 2026 kurekebisha mapungufu yote yaliyoonekana kwenye mradi wa jengo la makazi ya Mkurugenzi ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.

Naibu Waziri wa TAMISEMI (Elimu), Mhe. Reuben Kagilwa, amepokea maelekezo hayo na kusema kuwa Wizara itahakikisha yanafanyiwa kazi kwa wakati.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Mwanza, Mhe. Sima Constantine Sima, ameishukuru Kamati kwa ushauri wake wa kitaalamu na kuahidi kuwa Jiji litashirikiana kikamilifu kufikia malengo yaliyokusudiwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad