SERIKALI YAIMARISHA MIFUMO YA KIDIJITALI YA UFUATILIAJI WA MAGONJWA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 25 March 2026

SERIKALI YAIMARISHA MIFUMO YA KIDIJITALI YA UFUATILIAJI WA MAGONJWA

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeimarisha Mifumo ya Kidijitali ya Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko.

Hayo yamesemwa Jijini Arusha  na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Epidemiolojia  na  Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vida  Makundi Mmbaga katika Kikao Kazi  cha robo Mwaka cha Kutathmini Utekelezaji wa Kanuni za Afya za Kimataifa za Mwaka 2005 kilichoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu   pamoja na Shirika la Afya Duniani(WHO)kupitia Mradi wa  kupambana na magonjwa ya Mlipuko(Pandemic Fund).
"Serikali imeimarisha mifumo ya Kidijitali  ya Ufuatiliaji wa magonjwa,kila siku tunapata taarifa, tetesi za magonjwa ya aina yoyote na kuzifanyia kazi haraka"amesema Dkt. Mmbaga.

Aidha, Dkt. Mmbaga amesema   kuna timu mbalimbali ikiwemo za Ufuatiliaji, Udhibiti, Uelimishaji ambapo amesema kupitia Kikao hicho kimelenga kujitathmini katika utayari wa kujiandaa na kuzuia dharura za kiafya huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano utoaji wa taarifa, tetesi za magonjwa.
"Natoa wito kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa utoaji wa taarifa, tetesi za magonjwa na majanga yoyote yasiyo ya kawaida kwa kupiga 199 bila malipo ambayo ni namba mahsusi iliyojumuishwa  katika Mfumo wa  Ongea na Waziri"amesema Dkt.Mmbaga.

Halikadhalika, Dkt.Mmbaga amesema Ufuatiliaji wa Magonjwa huanzia katika ngazi za chini kabisa kwenye jamii kuanzia mwananchi mmojammoja, walimu wa shule,Wataalam mbalimbali ikiwemo wataalam wa mifugo na  Wataalam wa Tiba Asili .

"Tuna ushirikiano mzuri na wataalam wa tiba asili ambapo wanapoona dalili za mgonjwa hutoa taarifa kupitia kwa viongozi wa Serikali za mitaa na sisi huwa hatupuuzi taarifa yoyote tunayopokea"amesema.
Afisa wa Utayari na Udhibiti wa Dharura na Majanga kutoka Shirika la Afya Duniani(WHO) Tanzania Dkt. Faraja Msemwa amesema kupitia Mradi wa Pandemic Fund umesaidia katika ushirikishaji wa pamoja na kufanya Tathmini ya Kanuni za Afya za Kimataifa bila kusahau ngazi zote za Serikali.

Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu) Mwanaisha Mrisho amesema Kikao hicho kina umuhimu mkubwa katika kujiandaa namna gani ya kukusanya taarifa za awali katika kupambana na magonjwa ya mlipuko ambapo dhana ya afya moja husaidia ukusanyaji wa taarifa kutoka sekta mbalimbali mfano kukabiliana na magonjwa yanayotoka kwa Wanayama kwenda kwa binadamu.

Mratibu wa Huduma za Kinga na Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya, Zanzibar Yahya Mselem   amesema Kikao hicho ni taswira muhimu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Udhibiti wa Magonjwa ya Mlipuko.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad